HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, July 12, 2012

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi azindua Miongozo ya Udhibiti Ubora wa Elimu ya Juu itolewayo na vyuo vikuu nchini mjini Dodoma leo

Na Lydia Churi, MAELEZO-Dodoma

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa leo amezindua Miongozo ya Udhibiti Ubora wa Elimu ya Juu itolewayo na vyuo vikuu nchini iliyoandaliwa na Tume ya vyuo vikuu Tanzania..

Akizindua Miongozo hiyo katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, Waziri Kawambwa alisema Tume ya vyuo vikuu imepata mafanikio makubwa katika jitihada za kuboresha elimu ya juu nchini.

Alisema miongozo hii imeandaliwa wakati muafaka ambapo taasisi za elimu ya juu zinakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na maendeleo ya elimu ya juu kitaifa, kikanda na kimataifa.

Alisema miongozo iliyozinduliwa inalenga kudhibiti ubora wa elimu ya juu katika kuhakikisha kuwa programu za masomo zinazotolewa zinaandaa wahitimu wenye sifa na uwezo wa kuhimili ushindani katika soko la ajira.

Miongozi hiyo pia itahakikisha kuwepo na mfumo mzuri na usimamizi wa rasilimali watu katika taasisi za elimu ya juu hapa nchini na mwongozo sahihi wa jinsi ya kuanzisha taasisi za elimu ya juu. Awali yalikuwepo malalamiko kutoka kwa wadau kuhusu kutokuwepo kwa miongozo inayokidhi mahitaji muhimu katika usimamizi wa rasilimali watu katika taasisi za elimu ya juu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo miongozi hiyo pia itahakikisha kunakuwa na utaratibu stahili wa uahamisho wa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka programu moja ya masomo kwenda nyingine au kutoka taasisi moja kwenda nyingine.

Alisema kutokana na kukua kwa sekta ya elimu ya juu nchini, zimejitokeza taasisi nyingi zinazotoa huduma zenye ukubwa na michepuo tofauti ambapo tofauti hizo zinaonekana katika ngazi za vyuo vikuu vishiriki, skuli, vitivo, idara na vitengo vya elimu ya juu hali inayohitaji kuwepo kwa miongozo na vigezo ili kubaini muundo na hadhi ya ngazi mbalimbali za kiutawala katika taasisi za elimu ya juu.

Alisisitiza kuwa miongozo hii itakuwa na manufaa kwa watanzania endapo kutakuwa na ushirikiano kati ya Tume ya vyuo vikuu Tanzania na Taasisi za Elimu ya juu nchini pamoja na wadau wote wa elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad