HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 18, 2016

SERIKALI, KAMPUNI YA UJERUMANI WAJADILI ZAIDI UJENZI KIWANDA CHA MBOLEA

 Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mbele) akielezea jinsi Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilivyojipanga kutekeleza ujenzi wa Mradi wa Kiwanda cha Mbolea wilayani kilwa. Balozi wa Denmark Nchini, Einar H. Jensen (kulia kwa Dkt. Pallangyo), Ujumbe kutoka Kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH Ujerumani, Viongozi Waandamizi kutoka Wizarani pamoja na Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wakimsikiliza Dkt. Pallangyo.
 Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (mbele) akiwakilisha kabrasha ya kanuni za bei ya Gesi asilia kwa Balozi wa Denmark Nchini, Einar H. Jensen (mbele) wanaoshuhudia katika picha ni wajumbe kutoka Taasisi za Serikali pamoja na Ujumbe kutoka Kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH kutoka Ujerumani.
 Balozi wa Denmark Nchini, Einar H. Jensen (aliyenyanyua mikono) akielezea mpango wao wa kujenga kiwanda cha mbolea wilayani Kilwa kwa washiriki kutoka upande wa Serikalini (hawapo pichani) wanaoonekana pichani ni Ujumbe kutoka kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH kutoka Ujerumani.
Viongozi Waandamizi kutoka Serikalini wakimsikiliza Meneja wa Biashara ya Gesi (Downstream) kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert Simon wakati akielezea jambo katika kikao hicho.

Na Rhoda James
Serikali ya Tanzania na kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH kutoka Ujerumani wamekutana kwa mara nyingine na kujadili mambo mbalimbali ikiwemo namna ya kutatua changamoto zilizopo katika ujenzi wa Mradi wa kiwanda cha Mbolea wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi.
Katika kikao hicho ambacho kimefanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam, na ni mwendelezo wa vikao vya aina hiyo vilivyotangulia, Naibu katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi na utambuzi wa bei ya kuuza  gesi kwa kiwanda hicho.
Dkt. Pallangyo alifafanua kuwa, utaratibu wa kupata ardhi kwa ajili ya Mradi huo unaendelea vizuri kwani tayari Wananchi wamepata fidia ili kupisha Mradi huo na kufikia Januari, 2017 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) watakuwa na hati mpya itakayoruhusu Kampuni ya Ferrostaal kuanza maandalizi ya ujenzi wa kiwanda hicho.
Pamoja na hilo pia Dkt. Pallangyo alisema kuwa bei ya gesi inajadiliwa na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mdhibiti wa Mkondo wa Juu wa Shughuli za Mafuta (PURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), wazalishaji wa gesi (Upstreamer) na watumiaji wa gesi (Downstreamer) ili kujua bei halisi ya kuuza gesi hiyo kwa kampuni ya Ferrostaal kwa kuwa inatarajia kutumia gesi katika uzalishaji wa mbolea hiyo.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark Nchini , Einar H. Jensen alisema kuwa, ni vema Bodi ya TPDC ikakamilisha utaratibu wa makubaliano ya ubia (Joint Venture Agreement) kati yao na TPDC ili kuharakisha uanzishwaji wa utekelezaji wa mradi huo.
Ujenzi wa Mradi huo wa mbolea utashirikisha Kampuni tatu ambazo ni Ferrostaal Industrial GmbH ya Ujerumani, Fauji Fertilizer ya Pakistani na Haldor Topsoe ya Denmark pamoja na TPDC. 
Kikao hicho kilishirikisha wawakilishi kutoka Kampuni ya Ferrostaal Industrial GmbH, Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini pamoja na TPDC.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad