HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 16, 2016

MHE. GAMBO AWATAKA WAFADHILI KUTOA CHAKULA MASHULENI

Na Nteghenjwa Hosseah - Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amewataka wafadhili na wadau wa watoto kubuni miradi inayoendana na kusaidia  Mpango wa Serikali wa Elimu bure kwa shule za Msingi na Sekondari  ili kupunguza changamoto zinazojitokeza kwa sasa na kuuwezesha mpango huu kutekelezwa  kwa mafanikio makubwa.

Mhe. Gambo ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa kushirikishana tuliojifunza wakati wa utekelezaji wa mpango wa pamoja tuwalee uliotekelezwa kwa miaka sita kwenye Kanda ya Kaskazini  na ambao kwa sasa umemaliza muda wake ulifanyika kwenye Hotel ya Mt Meru Jijini hapa.

Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu wa Mkoa amesema kazi kubwa imefanyika wakati utekelezaji wote wa mradi  na mafanikio yake tumeonekana kwani watoto wamefikiwa na kusaidiwa kutoka katika mazingira hatarishi yaliyokuwa yanawakabili na wengine kupatiwa kadi za msamaha wa matibabu na zaidi mradi huu umekabidhiwa kwa Halmashauri husika ambazo  zitaendelea kusimamia na kutekeleza  mipango iliyowekwa chini ya mradi wa Pamoja Tuwalee.

Aliendelea kusema kuwa kukamilika kwa mradi huu katika awamu ya kwanza ni wazi kabisa kwamba ni maandalizi ya mradi mwingine ambao utakua na malengo yanayoshabihiana na programu ya awali hivyo ni vyema kwa kuwa walengwa bado ni watoto niwatake wadau kubuni miradi utakaolenga kusaidia Elimu bure na kwa kuwa watoto wote wanapata Elimu bure kupitia mpango huu basi ni vyema mkaelekeza nguvu kwenye utoaji wa Chakula kwa wananfunzi suala ambalo tumeona ni changamoto kwa watoto wetu.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la WEI – Bantwana “World Education Inc” Bi. Gill Gap alisema wanajivunia kuwa Taasisi iliyofanikisha utekelezaji wa mradi wa pamoja kwa ushirkiano wa Serikali ya Tanzania katia utekelezaji wa mradi pamoja na Serikali ya Marekani kwa ufadhili mradi huu. Pamoja Tuwalee ilikuwa maalumu kuwalinda watoto walio katika mazingira hatarishi  na kutoa Elimu kwa wazazi walioathirika namna ya kuishi na watoto hao pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa Halmashauri kuendeleleza jitahada za mradi huu.

Jacklin Badi ni Mkurugenzi wa WEI – Tanzania anasema “Bantwana ni kitengo ndani ya  Shirika la WEI kinachohudumia watoto na hapa Tanzania tulianza  utekelezaji mwaka 2010 na mpaka sasa tumefanikiwa kuwafikia watoto 1,470,445 pamoja na wazazi wao na wameweza kupatiwa  huduma jumuishi za kuwasaidia na kuwalinda watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo ya Wanawake, watoto na vijana “Center for women, Children and Youth Development (CWCD) Bi. Hindu Ally Mbwego ambao ni watekelezaji wa mradi huu wa Pamoja Tuwalee kupitia mwamvuli wa WEI-Bantwana amesema wamefanikiwa kuwafika katika maeneo yote ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Karatu na Moshi  na wanajivunia mafanikio waliyoyapata kutokana na mradi huu.

Tumebadilisha maisha ya watoto na kuhakikisha usalama wao katika Jamii wanazoishi, tumewatambua wazazi wenye watoto walioathirika na kuwapa elimu ya jinsi ya kuwafahamisha watoto wenye hali hiyo na namna ya kuishi nao ili waweze kukua katika malezi bora na afya njema sanjari na kupata Elimu alisema Bi. Hindu.

Mradi wa pamoja Tuwalee ni mpango wa Kitaifa wa miaka mitano uliotekelezwa na fedha za  mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupunguza makali ya virusi vya ukimwi kwa waathirka kupitia Shirika la Misaada la Marekani la USAID na kutekelezwa  na WEI-Bantwana pamoja na Kituo cha maendeleo ya Wanawake, watoto na vijana kilichopo Jijini Arusha.
    Mkurugenzi wa WEI-TANZANIA Bi. Lilian Badi (aliyesimama) akielezea mafanikio ya Mradi wakati wa Mkutano wa kuhitimisha mradi wa Pamoja Tuwalee.
  Mkurugenzi Mkuu wa World Education Inc Bi.Gill Garb akitoa taaria ya utekelezaji wa mradi wa Pamoja Tuwalee kupitia WEI-Bantwana.
 Mwakilishi wa US-AID Tanzania Bi. Maria Busquets akielezea namna ambavyo Shirika lake limefanikisha utekelezaji wa mradi wa Pamoja Tuwalee.
   Mkuu wa Mkoa wa Arusha akizungumza na wadau wa Mkutano 
 Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo ya Wanawake, watoto na vijana (CWCD) Bi. Hindu Ally Mbwego akielezea mafanikio ya mradi kupitia Kituo chake ambao ndio watekelezaji katika Halmashauri za Jiji la Arusha, Karatu na Moshi.
Picha ya pamoja ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha (katikati mbele), Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi waliotekeleza mradi huu, viongozi wa WEI, US AID, CWCD pamoja na  Wadau  wa watoto walioshirki katika Mkutano wa kuhitimisha mradi wa Pamoja Tuwalee.
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo(mbele kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa CWCD Bi. Hindu Ally Mbwego (kulia mbele) pamoja na baadhi ya watoto wa Pamoja Tuwalee.
    Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (Pili kushito) kwenye picha ya pamoja na wadau waliotekeleza mradi wa Pamoja Tuwalee
 Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (katikati) akiwa na wataalam kutoka Halmashauri ya Korogwe waliofanikisha utekelezaji wa mradi wa Pamoja Tuwalee.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad