Na Asteria Muhozya, DSM
Wizara ya Nishati na Madini, imeandaa Mkutano ambao pamoja na
masuala mengine utapokea Taarifa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi
Bandari ya Tanga, ambao utahudhuriwa na Mawaziri wanaosimamia sekta
hiyo kutoka Uganda na Tanzania.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Jijini Tanga tarehe 24 hadi 26,Oktoba,
2016, utatanguliwa na mkutano wa Wataalam kutoka Serikali ya Tanzania
na Uganda na kisha kufuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wa sekta
hizo, na tarehe 26 Oktoba, 2016, utafanyika Mkutano wa Mawaziri wa nchi
husika.
Mbali na Wataalam kutoka Tanzania na Uganda, mkutano huo pia
utashirikisha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Wawekezaji katika mradi
huo kutoka Kampuni za Total E&P ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza,
China National Offshore Oil Company (CNOOC) na kampuni za Mafuta za
Taifa za Tanzania na Uganda.
Mradi wa bomba hilo una urefu wa kilomita zipatazo 1,443 kutoka Hoima
nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga. Bomba hilo linatarajiwa kupita katika
mikoa ya Kagera, Geita, Tabora, Shinyanga Dodoma na Tanga.
Mradi huo ambao uliridhiwa na Baraza la Mawaziri kutekelezwa nchini
Tanzania mnamo tarehe 29/09/2016, katika kikao kilichoongozwa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, utakua
na manufaa makubwa kwa Tanzania kwa kuongeza kasi ya kukua
kiuchumi.
Bandari ya Tanga itapata fursa za kuongeza kiwango cha kufanya biashara
na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi na hivyo kuweza kufungua mkuza
wa kiuchumi baina ya Mikoa ambayo bomba hili litapita na nchi Jirani za
Afrika Mashariki.
Mradi huo unaotajwa kuwa mradi mwingine wa kihistoria, utagharimu kiasi
cha Dola za Marekani takribani Bilioni 3.5, ambapo utakapokamilika
unatarajiwa kuwa na uwezo wa kusafirisha jumla ya mapipa Laki Mbili
(200,000) kwa siku. Mradi utakua na Manufaa kwa Taifa ikiwemo kutoa
ajira za muda mfupi na mrefu.
No comments:
Post a Comment