HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 13, 2016

Tanzania na China zasaini Mkataba kusaidia sekta za maendeleo nchini


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Charles Mwijage akizungumza katika mkutano kati yake na Naibu wa Viwanda wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Dkt. Qian Keming.Mazungumzo yao yalijikita katika kuboresha mahusiano kati ya Tanzania na China katika kuboresha miundombinu.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Dkt. Keming wakimsikiliza kwa makini Dkt. Mwijage hayupo pichani.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji wakisaini Mkataba wa Makubaliano ya Kushirikiana katika masuala ya uchumi na teknolojia.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda (wa kwanza kushoto), Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Ramadhani Muombwa Mwinyi (katikati), na Mwakilishi kutoka Kituo cha Uwekezaji wa Tanzania kwa pamoja wakishuhudia uwekwaji saini katika mkataba huo.

Dkt. Mwijage na Dkt. Keming wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mkutano.

Serikali ya Watu wa China imeahidi kuipatia Tanzania msaada wa fedha wa kiasi cha Shilingi bilioni 97 kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb) baada ya kukutana na ujumbe kutoka China unaongozwa na Naibu Waziri wa Biashara wa nchi hiyo, Mhe. Dkt. Kian Keming.

Dkt. Kian na ujumbe wake upo nchini ambapo pamoja na mambo mengine walishiriki kikao cha tano cha Kamati ya pamoja ya Uchumi, Biashara, Uwekezaji na Ushirikiano wa Kiteknolojia kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mhe. Mwijage alieleza kuwa katika kikao hicho walijadili masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika viwanda, miundombinu na nishati. Alisema Serikali ya awamu ya tano imeweka mkazo katika maeneo hayo ili kufikia lengo la nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Alieleza kuwa katika harakati za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020, viwanda viwili vya chuma na marumaru vilivyojengwa na wawekezaji kutoka China vinatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao. Kiwanda cha tatu kitaanza kujengwa na wawekezaji wa China muda wowote watakapopewa eneo kwa ajili ya ujenzi huo.

Kiwanda cha kwanza ni cha chuma kilichopo Mlandizi mkoani Pwani ambapo kitakapoanza kazi, kitazalisha tani 1,200,000 za chuma kwa mwaka. Aidha, kiwanda kingine cha marumaru kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kinatarajiwa kuingiza pato la Dola za Marekani nilioni 150 kwa mwaka, kitakapoanza uzalishaji.

Kiwanda kinachosubiri kujengwa ni cha nguo ambacho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita milioni 240 kwa mwaka. Mhe. Waziri alieleza kuwa juhudi za kupata ekari 700 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho kwenye Wilaya ya Mkuranga zinaendelea na hivi karibibuni eneo hilo litakabidhiwa kwa wawekezaji hao.

Kwa upande wake, Dkt. Kian aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuwa China itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania ya kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Aidha, aliwakaribisha makampuni ya Tanzania kushiriki maonesho ya biashara yanayofanyika nchini China ili kuzitangaza bidhaa za Tanzania kwa madhumuni ya kupata soko nchini humo.

Mawaziri hao wawili waliweka saini Mkataba wa Makubaliano ya Kushirikiana katika masuala ya uchumi na teknolojia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad