HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, October 12, 2016

KAMPUNI YA MOLADI KUJENGA NYUMBA ZA WATUMISHI DODOMA.

 Waziri Mkuu Kassim Majiliwa amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Molad Tanzania Bwana Abeid Abdallah ambaye kampuni yake inajishughulisha na ujenzi wa nyumba za kisasa kwa gharama nafuu Waziri mkuu ameikaribibisha kampuni hiyo kujenga nyumba za watumishi Mkoani Dodoma mazungumzo hayo yamefanyika ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam
Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Molad Bwana Abeid Abdallah akimuonyesha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa baadhi ya picha na michoro ya nyumba za kisasa na zabei nafuu zinazo weza kujengwa Dodoma Picha na ofisi ya Waziri Mkuu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameikaribisha kampuni ya ujenzi ya Moladi Tanzania ielekeze nguvu zake Dodoma ambako kuna mahitaji makubwa ya nyumba za watumishi.

“Natambua kuwa mnatumia teknolojia ya kisasa na ujenzi wa nyumba zenu unachukua siku chache sana. Ninawaencourage mje Dodoma ambako kuanzia Machi mwakani, watumishi wengi wataanza kuhamia huko,” amesema.

 Waziri Mkuu ametoa wito huo leo mchana (Jumatano, Oktoba 12, 2016) wakati akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Abeid Abdallah ambaye alifika ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salaam na kumuonyesha ramani ya nyumba za watumishi ambazo wanazitumia.

Waziri Mkuu amesema Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina maeneo ambayo imeyatenga rasmi kwa ajili ya viwanja vya makazi na anaamini katika muda wa miezi miwili wanaweza kujenga nyumba za kutosha watumishi wanaotarajiwa kuhamia katika awamu ya pili.

“Nimeangalia michoro yenu, nyumba za vyumba vitatu vya kulala zina hadhi ya kukaa hata wakurugenzi; na watumishi wa kawaida wanaweza kumudu zile za vyumba viwili vya kulala… ninawatia moyo mwende haraka Dodoma na wale ambao wako serious wataleta maombi yao mara moja,” amesema.

Waziri Mkuu amesema amefarijika kuona kuwa size ya ramani zao inatosha kwenye kiwanja cha ukubwa wa mita za mraba 550 ambacho ni high density na watumishi wengi wanaweza kumudu kuvinunua.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo, Bw. Abdalla amemweleza Waziri Mkuu kwamba nyumba ya ukubwa wa vyumba vitatu vya kulala, yenye sebule, jiko, stoo na choo inatosha eneo la mita za mraba 94 tu.

“Kati ya vyumba hivyo vitatu, kimoja ni master, pia kuna sebule, chumba cha kulia na kibaraza. Hii inaanzia shilingi milioni 35 hadi milioni 41 kutegemea na aina ya vifaa unavyoweka kwenye umaliziaji. Lakini tukiongeza na servant quarter utalazimika kulipia shilingi milioni 7 ambapo unapata vyumba viwili na choo na bafu ndani,” amesema.

“Kimsingi, ni lazima tutaweka madirisha, milango, vyoo, masinki ya bafuni na jikoni, tiles (na mtu anaruhusiwa kuchagua za China, Italy au Spain),” ameongeza.

Akifafanua kuhusu nyumba yenye vyumba viwili vya kulala, Bw. Abdalla amesema nayo pia ina sebule, jiko, stoo na choo kimoja na inatosha eneo la mita za mraba 54. Amesema nyumba hizo zinaanzia sh. milioni 20 hadi 25 kutegemeana na aina ya vifaa vinavyowekwa kwenye umaliziaji.

Amesema ujenzi wa nyumba moja unachukua wiki sita na kama viwanja viko eneo moja au jirani, wanaokoa muda wa siku tatu hadi tano kwa kila nyumba. “Tunajenga ukuta kwa kumwaga theluji isiyochanganywa na kokoto ambayo ni mchanganyiko wa saruji, mchanga na kemikali. Inakauka baada ya saa saba na ukuta wetu ni imara mara nne zaidi ya ukuta uliojengwa na tofali la zege.”

Teknolojia yetu inawezesha ukuta wa nyumba nzima kukamilika ndani ya siku sita, nyumba zetu zinastahimili matetemeko, vimbunga na ujenzi wake unapunguza gharama za ujenzi kwa asilimia 40.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa nyumba hizo, Bw. Abdalla amesema wana mikataba na mabenki kwa hiyo wanaweza kujenga nyumba na kuziuza mara moja lakini pia wananchi wanaweza kuingia mikataba na mabenki na kulipia kidogo kidogo katika muda maalum (mortgage).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.
JUMATANO, OKTOBA 12, 2016.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad