HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, September 24, 2016

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI, PROFESA SOSPETER MUHONGO AMEMTAKA MKANDARASI WA KAMPUNI YA STATE GRID COMPANY ATEKELEZA MRADI WA UMEME VIJIJINI (REA II) WILAYANI KAKONKO MKOANI KIGOMA.

 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (aliyeshika kipaza sauti) akizungumza na wananchi wa eneo la mradi.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimuelekeza jambo Mkurugenzi wa Kampuni inayotekeleza mradi wa Umeme Vijijini Mkoani Kigoma ya State Grid, Wilboad Mutabuzi kulia.
Wananchi wa Wilaya ya Kakonko wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua Mradi wa Umeme Vijijini kwa Mkoa wa Kigoma

WITO huo umetolewa jana wilayani humo wakati alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) Mkoani Kigoma ambapo alibaini changamoto mbalimbali ikiwemo ya nguzo za umeme kusimikwa vibaya bila kuzingatia utaalamu hasa ikizingatiwa kuwa maeneo hayo hua na upepo mkali unaoweza kusababisha nguzo hizo kuanguka.

Katika ziara hiyo, Profesa Muhongo alipatiwa taarifa na Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Col. Hosea Ndagala ambaye alimueleza kutoridhishwa na namna mradi huo unavyotekelezwa ikiwemo uduni katika usimikaji wa nguzo za umeme.

Alisema baadhi ya nguzo hizo zimeanza kuinama kutokana na upepo pamoja na kutosimikwa vizuri hali inayoweza kusababisha madhara kwa Wananchi wa eneo hilo endapo nguzo hizo zitadondoka.

Kufuatia taarifa hiyo na ukaguzi alioufanya kwenye eneo la mradi, Waziri Muhongo aliagiza hadi kufikia mwisho wa Mwezi huu Mradi huo uwe umekabidhiwa kwa Meneja wa TANESCO Kigoma na kwamba kabla ya kupokelewa Mkuu wa Wilaya naye athibitishe kuridhishwa utekelezaji wake ikiwemo kurekebisha kasoro zilizobainika ili wananchi wanufaike na mradi ulio katika ubora unaotakiwa.

Profesa Muhongo alisema endapo Mkandarasi atashindwa kutatua changamoto hizo na kasoro zilizo jitokeza katika mradi huo hatoruhusiwa kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa REA III ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya  Awamu hii ya pili kukamilika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya State Grid, Wilboad Mutabuzi alisema usambazaji umeme mkoani humo umekamilika kwa asilimia 98 na huku akiahidi kuhakikisha anashughulikia kasoro zilizobainika ili akamilishe mradi kwa wakati na wenye ubora unaokubalika.

Mutabuzi alisema gharama za mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kwa mkoa wa Kigoma ni shilingi bilioni 23 na kwamba katika Wilaya ya Kakonko vijiji saba vimefaidika na mradi huo.

Alisema  changamoto kubwa iliyojitokeza ni muitikio mdogo wa Wananchi kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema kutokana na muitikio wa wananchi kuwa mdogo imesababisha kushindwa kufikia lengo ambapo kwa Mkoa mzima wa Kigoma lengo lilikuwa ni kuwaunganishia huduma ya umeme wateja wapatao 11,000  lakini hadi sasa ni wateja 7,000 tu ndio waliopatiwa huduma husika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad