HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 27, 2016

NHIF ILIVYOSHIRIKI MECHI YA WABUNGE

Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga alipotembelea banda la upimaji afya katika Uwanja wa Taifa wakati wa Mechi ya Wabunge wa Simba na Yanga. 

Na Grace Michael

WAZIRI Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwahudumiwa wanachama wake lakini pia kuendesha shughuli za upimaji wa afya bure katika maeneo mbalimbali.

Pamoja na pongezi hizo, ameutaka Mfuko huo kuangalia namna ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi katika suala la upimaji wa afya ili kila mmoja ajue hali ya afya yake.

“Kwanza niwapongeze tu kwa kazi kubwa mnayoifanya hapa ya kutupima afya zetu...hakikisheni shughuli hizi zinafanyika mahali pengi zaidi kwani kwa sasa kuna mwamko mkubwa sana wa wananchi kupima afya zao, hata pale bungeni leteni huduma hizi wakati wa bunge ili waheshimiwa wabunge nao wapate fursa hii,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuwa msaada mkubwa katika usimamizi na utoaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wake pamoja na uboreshaji wa huduma za matibabu.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujiunga na huduma za Mfuko ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote wanapohitaji lakini pia kuhakikisha wanatumia fursa za upimaji wa afya zinapokuwa katika maeneo yao.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nape Nnauye akizungumzia zoezi la upimaji lililofanywa na NHIF uwanjani hapo, alisema kuwa ni jambo zuri kwa kuwa mbali na watu kujua hali ya afya zao lakini watapata elimu ya namna ya kujiunga na huduma za Mfuko.

Alitoa wito kwa vijana kuhakikisha wanajenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujua hali zao kwa kuwa ndio nguvu kazi inayotegemewa katika uzalishaji wa Taifa hili.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema kuwa, Mfuko umeendesha zoezi hilo uwanjani hapo kwa lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali hususan katika kushughulikia tatizo la janga la tetemeko lililotokea mkoani Kagera.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Nape Nnauye akipima uzito kabla ya mechi kuanza.
Katibu Mkuu wa Wizara y Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Gabriel akipima kiwango cha sukari katika banda la NHIF.
Mbunge wa Sengerema Bw. William Ngeleja akipima uzito kabla ya mtanange kati ya wabunge wa Yanga na Simba.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga akipokea cheti kutoka kwa Waziri Mkuu ambacho kinautambua mchango wa Mfuko katika janga la tetemeko lililotokea mkoani Kagera.
Waziri wa Habari Bw. Nape Nnauye akiongozana na Ofisa Masoko na Elimu kwa Umma wa NHIF, Bi. Grace Michael kuelekea kwenye banda la Mfuko huo ambalo liliendesha upimaji wa afya kwa wananchi wote waliofika uwanjani hapo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa mfuko huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad