HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 25, 2016

MADAKTARI WANAOMILIKI MADUKA YA DAWA NJE YA HOSPITALI WATAKIWA WACHUNGUZWE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk Beatrice Byalugaba kufanya uchunguzi na kubaini madaktari wa hospitali ya wilaya ya Mafia wanaomiliki maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo na kuwachukulia hatua.

Amesema ameshangazwa kukuta maduka ya dawa yanayomilikiwa na madaktari nje ya hospitali hiyo kwani tayari Serikali ilishaagiza kuondolewa kwa maduka ya madaktari karibu na hospitali wanazofanyia kazi.

Waziri mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 24, 2016) wakati alipotembelea hospitali ya wilaya ya Mafia katika siku ya pili ya ziara yake wilayani mafia.

Kuhusu tatizo la upungufu wa dawa hospitalini hapo amemuagiza Dk. Beatrice kufanya utafiti wa aina ya magonjwa yanayowasumbua wananchi wa wilaya hiyo ili wanapoagiza waagize dawa nyingi za kutibu magonjwa hayo.

Pia aliwataka watumishi wa hospitali hiyo wajitahidi kuwahudumia vizuri wagonjwa licha ya uchache wao. Lengo ni kuhakikisha wanapunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amewahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kuwa na uhakika wa kupatiwa matibabu bure kwa kipindi cha mwaka mzima.

Awali Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Joseph Mziba alisema mwamko wa wananchi kujiunga na mfuko wa CHF ni mdogo jambo linalokwamisha upatikanaji wa huduma za afya wilayani Mafia. Jumla ya wananchi waliojiunga na CHF ni  watu 6,000 kati ya watu 50,000.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Bw. Eric Mapunda ameiomba Serikali kutoa kibali kwa halmashauri kununua dawa ambazo zinakosekana MSD kwenye soko moja kwa moja bila ya kupitia utaratibu wa manunuzi.

"Kuna wakati tunakosa dawa MSD na kulazimika kununua kwa mawakala kwa kufuata taratibu ya manunuzi. Tunalazimika kununua boksi moja la ambapo boksi moja la panadol linauzwa sh. 20,000 na tukinunua moja kwa moja sokoni bila ya kufuata utaratibu huo boksi hilo hilo tunalipata kwa sh. 8,000,”alisema

Baadhi ya wananchi waliokuwepo hospitalini hapo walieleza malalamiko yao kuhusu lugha chafu na dharau inayotolewa na baadhi ya madaktari na wauguzi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad