HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 8, 2016

MRADI WA NG'OMBE KUWANUFAISHA WANAWAKE WA VIJIJINI WILAYANI NGORONGORO

Wanawake wenye kipato cha chini kutoka vijiji vinne vya wilaya ya Ngorongoro wamekabidhiwa Ng’ombe ili kuwasaidia kuondokana na umasikini.

Wanawake hao wapatao 28 kutoka vijiji vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu walichaguliwa kulingana na hali yao ngumu ya maisha inayowapelekea wakati mwingine kunyanyaswa kijinsia kupitia mfumo dume. Wanawake wengine 15 watakabidhiwa Ng’ombe wao mnamo mwezi Machi mwaka huu kufanya idadi ya wanufaika kufikia 43.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Enguserosambu yalihudhuriwa na  Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, viongozi mbalimbali wa vijiji, pamoja na wakazi wa eneo hilo.

Akikabidhi Ng’ombe hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Hashim Mgandilwa aliwataka wanawake hao kuhifadhi vizuri mifugo hiyo ili iwasaidie kujikwamua kiuchumi kwa kuuza bidhaa zitokanazo na Ng’ombe ikiwemo maziwa. Aidha Mkuu huyo wa wilaya alitoa rai kwa viongozi wa vijiji hivyo kuhakikisha kwamba inapotokea misaada kama hii iwanufaishe walengwa ambao mara nyingi ni watu maskini ili kuwaepusha na balaa la njaa.

Ng’ombe hao wametolewa kama msaada na shirika la Oxfam kupitia wadau wake shirika la PALISEP.

Akizungumza katika hafla hiyo Meneja wa programu ya wafugaji wa Shirika la Oxfam ndugu Laurent Wambura alisema shirika lake limefanya hivi ili kuwainua kiuchumi wanawake wenye kipato cha chini na kubadilisha mtazamo wa jamii ione kwamba hata wanawake wanaweza kumiliki mali ikiwemo mifugo na kubadilisha kabisa maisha yao.

Naye Mkurugenzi wa shirika la PALISEP Robert Kamakia alisema lengo la mradi huo ni kuwezesha upatikanaji wa lishe bora na maziwa kwa familia zisizo na uwezo pamoja na kupunguza makali ya magonjwa kwa watoto kama vile utapiamlo.

Hii sio mara ya kwanza kwa shirika la Oxfam kugawa Ng’ombe katika wilaya ya Ngorongoro, mnamo mwaka 2014 wanawake wapatao 66 walinufaika na mradi huu kwa kugawiwa ngo’mbe mmoja jike kila mmoja huku viongozi wa vijiji vinne vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu wakikabidhiwa madume 6 wa mbegu kama sehemu ya kuboresha mifugo ili kukidhi mahitaji ya soko. Ndama wote wanaozaliwa kama uzao wa kwanza wa Ng’ombe hawa hugawiwa kwa wanawake wengine wenye kipato cha chini hivyo kunufaisha jamii kubwa.
  Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Mhe. Hashim Mgandilwa akiongea na wakazi wa Ngorongoro wakati wa kukabidhi Ng'ombe hao 
 Robert Kamakia kutoka shirika la PALISEP akimkabidhi Mkuu wa Wilaya Mhe. Hashim Mgandilwa risala kuhusu makabidhiano hayo. Theresia Irafay, Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Ngorongoro akizungumza wakati wa ugawaji wa Ng'ombe hao.
 Laurent Wambura kutoka shirika la Oxfam akizungumza wakati wa ugawaji wa Ng'ombe hao.
Mh. Hashim Mgandilwa, Mkuu wa wa Wilaya ya Ngorongoro akikabidhi Ng'ombe kwa wanawake wa wilaya ya Ngorongoro.
 Wakazi wa vijiji vya Enguserosambu, Naan, Ng’arwa na Orkiu Juu wakihudhuria ugawaji wa Ng'ombe uliofanyika katika kijiji cha Enguserosambu.
 Picha ya pamoja 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad