HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, February 8, 2016

MKUTANO WA WADAU WA UWEZESHAJI KUFANYIKA KESHO FEBRUARI 9 MWAKA HUU.

BARAZA LA TAIFA LA UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
 MKUTANO WA WADAU WA UWEZESHAJI UTAKAOFANYIKA TAREHE 9/02/2016.
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lilianzishwa mwaka 2005 kwa Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Sheria na. 16 ya Mwaka 2004) chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Baraza ni chombo cha juu kitaifa cha kuratibu, kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004.
Katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji, Baraza limeshaandaa Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Mwongozo wake unaohusisha sekta zote nchini.

 Ili kufanikisha utekelezaji wa mkakati huo, Baraza limeandaa Mkutano wa Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao ni muundo rasmi katika kutekeleza Mkakati wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Mkutano huu ni sehemu ya Uratibu na utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji ambao unahusisha wadau mbali mbali ambao ni Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi.

Mkutano huu wa Wadau wa Uwezeshaji utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh Majaliwa Kassim Majaliwa (MB), tarehe 9/02/2016 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere.

MAJUKUMU YA BARAZA
                     i.        Kuandaa Mpango Mkakati wa Kisekta na kuhamasisha matumizi ya rasilimali kwa shughuli za uwezeshaji wananchi;
                    ii.        Kuhamasisha na kuhimiza uwekaji wa akiba, uwekezaji na ushirikishwaji makini wa wananchi kwenye shughuli za kiuchumi;
                   iii.        Kusimamia, kuongoza na kubaini vyanzo vya fedha kwa ajili ya Mfuko wa udhamini mikopo ya uwezeshaji ;
                   iv.        Kuwezesha na kuratibu mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi mbalimbali vya wananchi kutegemeana na mahitaji na changamoto zinazowakabili;
MALENGO YA MKUTANO WA WADAU WA UWEZESHAJI
  1. Kukutanisha wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kutoka sekta za umma na binafsi hapa nchini,
  2. Kujadili taarifa ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi;
  3. Kutambua  juhudi za wadau wanaotekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji;
  4. Kujaidili changamoto na kuibua mbinu bora za utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi;
  5. Kuhamasisha juhudi mbali mbali za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi,
MATARAJIO
Kupitia Mkutano huu wa Wadau wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Baraza lina matarajio yafuatayo;
i.        Kuanza rasmi kwa  Dawati la Uwezeshaji na Ushiriki wa Wananchi kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa, Wizara na Idara katika kufuatilia masuala ya Uwezeshaji, kuandaa taarifa na kuwasilisha katika kamati husika kwa maafikiano na kuwasilisha katika Baraza la Taifa la Uwezeshaji;
ii.        Taasisi za umma na binafsi kuwahudumia wananchi kwa ufanisi bila upendeleo pale wanapohitaji kuwezeshwa kupitia huduma wanazozitoa katika utendaji wao wa kila siku;
iii.        Kuratibu majukumu ya Uwezeshaji kwa kuzingatia uwajibikaji, uadilifu, uaminifu na kujali;
iv.        Kuchochea hamasa na kuhakikisha kuwa wananchi wanapewa upendeleo wa pekee kwa watoa huduma mbalimbali katika zabuni na miradi mikubwa katika maeneo yao pale wanapokidhi vigezo na masharti ya zabuni husika.
v.        Kila kiongozi kuhakisha kuwa rasilimali zilizotengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuwezeshaji wananchi kiuchumi zinaelekezwa katika miradi hiyo na kutumika kwa kuzingatia thamani ya pesa na miradi yenyewe;
Baraza linapenda kuwashukuru wadhamini wa Mkutano huu ambao ni (Mradi wa Ushindani wa Sekta Binafsi (Private Sector Competitiveness Project), World Vision Tanzania, Benki ya Maendeleo ya TIB (TIB Development Bank), Benki ya Posta, Benki ya CRDB, UTT Microfinance, Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF) na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad