Naibu mkurugenzi mkuu wa Benki M Bi. Jacqueline Woiso akiongea na waandishi wa habari leo hii katika
ukumbi wa Hyatt Regency juu ya maandalizi ya Rotary Dar Marathon 2015 ambayo huandaliwa na
Rotary klabu za Dar es salaam kwa kushirikiana na Benki M. Mbio na matembezi ya Dar Rotary
Marathon kwa mwaka huu zitafanyika katika viwanja vya Green, Oysterbay tarehe 14 October 2015.
Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa bodi ya Rotary Bi. Sharmila Bhatt, Mwenyekiti wa kamati ya
maandalizi Bi. Agnes Batengas, Makamu wa Raisi wa Rotary klabu Oysterbay Bi. Anne Saels na Rais wa
Rotary Klabu Dar North Bw. Masato Wassira.
baadhi ya washiriki wa Rotary Dar Marathon kutoka Malawi na Kenya wakifuatilia mkutano huo,
Marathon ya mwaka huu itajumuisha wakimbiaji kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Malawi, South Africa na
Ethiopia.
Mbio na matembezi ya hisani za Dar rotary marathon yanatarajiwa kufanyika siku ya jumatano tarehe
14.10.2015 hapa jijini Dar es salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa rais mstaafu mheshimiwa
Ally Hassan Mwinyi.
Mbio na matembezi hayo yameandaliwa na klabu sita za Rotary za hapa Dar es
salaam kwa kushirikiana na Benki M na kauli mbiu ya mwaka huu ni “kuponya maisha, badilisha jamii”
ambapo fedha zitakazochangishwa ziltaelekezwa katika ujenzi wa kituo cha afya hapa Dar es salaam.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana kuhusu maandalizi, mwenyekiti wa kamati ya
maandalizi Bi. Agnes Batengas alisema kuwa kamati yake imejiandaa vilivyo na maandalizi yote
yamekamilika, ikiwemo kupokea wakimbiaji kutoka nje ya nchi na washiriki wengine.
Aliongeza kuwa mbio hizo huwa zina lengo la kuchangisha fedha za kusaidia kupunguza changamoto
zinaoikabili jamii yetu, kama ilivyo mwaka huu ambapo tutajenga kituo cha afya.
Bi. Batengas alisema kuwa wanatarajiwa kuwa na washiriki wapatao zaidi ya 13,000 ambapo kutakuwa
na matembezi ya kilomita 5 kwa ajili ya familia, kilomita 9 na mbio za kilomita 21.1 nusu marathon,
halikadhalika kutakuwa na waendesha baiskeli.
Matembezi na mbio hizo zitaanzia na kuishia katika
viwanja vya Green, Oysterbay ambapo wakimbiaji na waendesha baiskeli wataanza saa 12 asubuhi na
watemebeaji wataanza saa 1 asubuhi. Barabara maarufu za jijini zitatumika ikiwemo Toure Drive, Chole,
Haile sellasie, Alli Hassan Mwinyi, Obama, Kivukoni, Ohio na Kenyatta.
Kuhusiana na usalama katika tukio hilo ambalo litahusisha maelfu ya watu, Bi. Batengas alisema
“tumekuwa tukifanya kazi kwa ukaribu sana na jeshi la polisi, hivyo jeshi la polisi limeshajipanga vilivyo
kwa ajili ya tukio hilo ili kuhakikisha kila kitu kinaisha kwa usalama”, alisema.
Naye naibu katibu mkuu wa chama cha riadha Tanzania Bi. Ombeni Zavala alisema kuwa mamlaka zote
zimehusishwa katika kuandaa tukio hili, “tumekuwa tukifanya kazi kwa kushirikiana na kamati ya
maandalizi ya Dar Rotary marathon kwa muda mrefu na tumekuwa tukihakikisha kila marathon
wanayoandaa inafanyika katika viwango vya kimataifa.
Mwenyekiti wa bodi ya Rpotary, Bi. Sharmilla Bhatt aliongeza kuwa Marathon ya mwaka huu itakuwa na wakimbiaji
kutoka kila pembe ya Africa. “Muitikio kutoka nchi za jirani ni mkubwa, wakimbiaji kutoka Kenya, Rwanda, Malawi,
Afrika Kusini na Ethiopia wamethibitisha kushiriki. Na tutaongeza nchi nyingi zaidi mwaka ujao wa 2016 kwa kuwa
umaarufu wa Dar Rotary marathon unazidi kuongezeka siku hadi siku na nchi nyingi ziko tayari kuleta wakimbiaji wao
maarufu kabisa kuja kushiriki. Jumla ya washiriki 13,000 wanatarajiwa kushiriki Marathon ya mwaka huu”.
Akichangia juu ya ushiriki wa Benki M katika mbio na matembezi haya, Naibu mkurugenzi mkuu wa benki hiyo Bi.
Jacqueline Woiso alisema kuwa wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali maendeleo ya jamii, hivyo
wamekuwa wakishirikiana na Rotary katika Rotary Dar marathon toka ilipoanzishwa mwaka 2009.
Aliongeza kuwa “ni sera yetu kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazoheshimika katika kuleta mageuzi kwa wahitaji
hapa nchini, tunaamini kabisa kuwa kwa pamoja tukishirikiana tutafanikisha ujenzi wa kituo hiki cha afya hapa Dar es
salaam. Hii ina maana kubwa sana kwetu kuiona sekta ya afya katika jamii yetu inapewa kipaumbele”.
Mbali na Benki M ambaye ndiye mdhamini mkuu, wadhamini wengine ni SBC (Pepsi), Spicenet, Soft tech, Toyota,
Ultimate Security, Security Printers, Copy Cat, ALAF, Azam Tv, BG Tanzania na Grand malt.
No comments:
Post a Comment