HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 5, 2015

Waziri Mkuu aitaka NHIF kuongeza bidii katika kutoa elimu ya Afya kwa Jamii

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akipatiwa maelezo ya huduma zinazotolewa katika banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko huo, Rehani Athumani, wakati alipotembelea Banda lao kwenye Maonyesho ya Nane nane, mkoani Lindi.
Waziri Mkuu akitoa maagizo kwa uongozi wa Mfuko wa kuongeza elimu hususan katika magonjwa ya unyanyapaa ndani ya jamii.
Mwanachama wa Mfuko akipata maelezo ya huduma zinazotolewa bandani hapo.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa Mfuko Rehani Athuman akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Waziri Mkuu.
Wananchi na wanachama wakifuatilia kwa makini elimu ya huduma zitolewazo na Mfuko.
Akina mama wakijisajili na Mfuko wa Afya ya Jamii.
Kitengo cha upimaji wa afya kikiendelea na kazi ya kuwahudumia wananchi.
Maofisa kutoka NHIF wakiwa katika picha ya pamoja.

Na Grace Michael, Lindi

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameuagiza uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa jamii namna ya kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa ambayo yanaleta unyanyapa ndani ya jamii.

Mbali na agizo hilo pia Waziri Mkuu alikiri kuridhishwa na jitihada za makusudi zinazofanywa na Mfuko huo ambazo zimesababisha mpaka sasa kuhudumia jumla ya asilimia 22.7 ya watanzania wote. Hayo aliyasema jana mkoani hapa wakati akitembelea Taasisi mbalimbali zilizoshiriki kwenye maonesho ya Kitaifa ya Nane Nane katika viwanja vya Ngongo.


“Kazi mayofanya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni nzuri mno, idadi ya Watanzania ambao mmeweza kuwafikia ni nzuri ikiwemo na mipango mliyonieleza hapa ya kuendelea kuongeza wigo wa wanachama… kwa upande wa elimu hasa hii mnayoitoa ya namna ya kuishi mtindo bora wa maisha na kuepukana na magonjwa ya kuambukiza mnafanya vizuri ila angalieni sasa na haya magonjwa mengine ambayo yanawafanya watu wanyanyapaliwe na jamii,” alisema Pinda.

Alisisitiza kuwa kutoa elimu juu ya magonjwa hayo yakiwemo ya ngozi itaisaidia jamii kwa kiwango kikubwa kuishi na kuwahudumia wagonjwa hawa kwa upendo na kuachana na unyanyapaa unaofanywa kwa baadhi ya wanajamii.

Waziri Mkuu Pinda alipata fursa ya kukagua huduma zote za Mfuko ambazo zinatolewa katika maonesho hayo ambazo ni pamoja na elimu kwa umma inayohusiana na huduma zinazotolewa, namna ya kujiunga na faida za mwanachama wa Mfuko. Huduma zingine ni upimaji wa saratani ya matiti, shinikizo la damu na kiwango cha sukari.

Awali Waziri Mkuu alipokea maelezo ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko na Utafiri Bw. Rehani Athumani ambaye alisema kuwa, Mfuko umejikita katika kuhamasisha Watanzania wajiunge na huduma zake ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wote.

Bw. Rehani alisema kuwa, Mfuko umeangalia makundi yote na kuweka taratibu ambazo zitawawezesha wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kuweza kunufaika na huduma za Mfuko. “Kwa sasa Mfuko unao mpango wa KIKOA ambao unawawezesha wajasiliamali kujiunga na Mfuko kwa gharama ndogo hivyo tunaamini kabisa wananchi wote watanufaika,” alisema Bw. Rehani.

Alisema kuwa kwa sasa Mfuko umesogeza huduma zake kwa wananchi kwa kuwa na ofisi kila Mkoa ambapo elimu ya afya inawafikia zaidi wananchi katika maeneo yote ya mijini na vijijini. Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mwantumu Mahiza alisema kuwa katika uongozi wake mkoani hapa atahakikisha asilimia kubwa ya wananchi wanajiunga na huduma za Mfuko ikiwemo na Mfuko wa Afya ya Jamii ili wananchi wa Lindi wawe na uhakika na matibabu.

“Nitashirikiana na Mfuko lakini pia nitahakikisha wananchi wanajua umuhimu wa suala hili…bila kuwa na uhakika wa matibabu hata shughuli za kiuchumi zinakwama hivyo kama Serikali lazima suala hili tulisimamie kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Bi. Mahiza.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuwa ukishiriki maonesho hayo kila mwaka ambapo katika maonesho ya mwaka jana, Mfuko uliibuka mshindi wa kwanza katika sekta ya utoaji huduma katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad