HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 4, 2015

BODI YA USAJILI WA WAHANDISI (ERB) YAKUZA AJIRA NCHINI.

Picha. Na.1. Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini Tanzania(ERB) Muhandisi Steven Mlope akiongea na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam kuelezea mafanikio ya Bodi hiyo katika kipindi cha miaka 10 hasa ukuzaji wa sekta ya ajira nchini Tanzania.

Picha na Aron Msigwa -MAELEZO
BODI ya Usajili wa Wahandisi nchini Tanzania (ERD) imefanikiwa kutengeneza ajira 1600 kwa Watanzania kufuatia usajili wa makampuni 160 ya ushauri wa kihandisi yaliyoanzishwa nchini kote nchini katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2005 hadi 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuelezea mafanikio ya Bodi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 Msajili wa Wahandisi nchini Tanzania (ERB) Muhandisi Steven Mlope amesema kuwa kwa kusajili makampuni 160 katika kipindi cha miaka 10 pia wamefanikiwa kusajili wahandisi wapatao 8496 ambao kwa ujumla wao wametengeneza ajira kwa Watanzania 256,480.

Amesema katika kipindi cha miaka 10 Bodi hiyo imefanikiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wahandisi waliosajiliwa kutoka 6868 waliokuwepo nchini Tanzania hadi 15,364 mwaka 2015.

Aidha Muhandisi Mlope amesema kuwa Fani ya Uhandisi nchini Imeendelea kukukua kutokana na uwepo wa wahandisi wa Majengo,wahandisi wa mazingira, Mifumo ya kompyuta na wahandisi wa mazingira wanaofanya kazi zao kwa kushirikiana.

Aidha, amesema kuwa Bodi ya Usajili wa Wahandisi kwa kuzingatia  sheria ya Bunge namba 15 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho, na sheria No.24 ya mwaka 2007 imepewa majukumu ya kuratibu na kusimamia mienendo na shughuli za Kihandisi zinazofanywa na wahandisi pamoja na makampuni ya ushauri wa kihandisi nchini.

Ameongeza kuwa kwa mujibu Sheria ni kosa kwa mtu binafsi,kikundi cha watu binafsi, kikundi cha watu au kampuni yoyote kutoka ndani na nje ya nchi kufanya shughuli za kihandisi bila kusajiliwa au kuwa na wahandisi wasiosajiliwa.

Ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2015 Bodi hiyo ilitoa onyo na adhabu mbalimbali ikiwemo kufuta usajili wa wahandisi 330 waliokiuka Sheria ya Bodi ya Usajili wa wahandisi.

Kwa upande wa shughuli za kihandisi katika ngazi ya wilaya kote nchini Muhandisi Mlope amesema kuwa kufikia mwaka 2015 hali imeendelea kuimarika licha ya kuwepo kwa changamoto ndogondogo.

Muhandisi Mlope amebainisha kuwa Bodi inaendelea kuratibu mpango wa Mafunzo (SEAP) wenye lengo la kuwajengea uwezo wahandisi wanaohitimu masomo katika  vyuo mbalimbali ili waweze kukidhi viwango kuwawezesha vya kuwawezesha kusajiliwa na Bodi hiyo.

"Mpango huu wa mafunzo unaofadhiriwa na Serikali kwa lengo la kuwajengea uzoefu wahitimu, kuwawezesha kuajiliwa na kupata uzoefu mapema umekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu"

Ametoa wito kwa wenye viwanda na makampuni kuwapokea na kuwaajili wahandisi waliosajiliwa na wale waliokula kiapo ili kazi wanazozifanya ziweze kukidhi viwango vilivyowekwa.

Pia amesema kuwa Bodi hiyo inaendelea kuwaendeleza wahandisi wataalaam waliopo nchini kwa kuandaa mihadhara na kozi fupifupi ambazo huendeshwa na vyuo vinavyotoa mafunzo ya kozi hiyo huku wao kama bodi wakitoa ithibati  na kuandaa makongamano ya wahandisi kila mwaka.

Amefafanua kuwa Septemba 3 mwaka huu Wahandisi watakuwa na Kongamano kubwa la mwaka litakalowakutanisha wahandisi wote nchini ili kuweza kukidhi matarajio ya Wananchi kufuatia wengi wao kuongeza uelewa juu ya matumizi ya wahandisi.

"Mwamko sasa umeongezeka kutokana na Serikali kuendelea kuweka mkazo katika masomo ya Sayansi na ujenzi wa maabara ili kuzalisha wataalam wa kutosha wenye viwango" Amesema.

Kuhusu maslahi ya wahandisi nchini amesema kuwa wao kama Bodi wanaishukuru Serikali kwa kuendelea  kuboreshaji maslahi yao na kusisitiza kuwa jambo hilo linaendana na mabadiliko ya uchumi yaliyopo ili kuwawezesha wataalam hao kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuheshimiwa na jamii wanayoitumikia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad