HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 3, 2015

WAZIRI WA UTALII NA MALIASILI MHE. LAZARO NYALANDU AFUNGUA MKUTANO WA UHIFADHI WA WANYAMAPORI TANZANIA

   WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akisalimiana na baadhi ya wadau wa masuala ya uhifadhi na utalii wakati alipofungua mkutano wa majadiliano kuhusu uboreshaji wa mfumo wa usimamizi na uendeshaji Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (WMA), ulioanza jana jijini Arusha.
 WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akifuatilia majadiliano wakati wa mkutano wa      wadau na viongozi wa Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori nchini (WMA), ulioanza jana jijini Arusha.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akizungumza na wadau na viongozi wa Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori nchini (WMA), ulioanza jana jijini Arusha kujadili uboreshaji mfumo wa usimamizi na uendeshaji jumuia hizo.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akisalimiana na mdau wa masuala ya utalii na uhifadhi nchini, Willy Chambulo, muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa majadiliano kuhusu uboreshaji wa mfumo wa usimamizi na uendeshaji Maeneo ya Jumuia ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania (WMA), ulioanza jana jijini Arusha.


KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO KATI YA WIZARA NA WMAs
UKUMBI WA NAURA SPRINGS, ARUSHA,
TAREHE 2 & 3 JULAI, 2015.

Mhe. Mahmood Mgimwa - Naibu Waziri,Wizara ya Maliasili na Utalii;
Dkt. Adelherm Meru         - Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii;
Bw. Herman Keraryo        - Mkurugenzi, Idara ya Wanyamapori;
Dkt. Simon Mduma            - Mkurugenzi Mkuu,Taasisi ya Utafiti wa
                                           Wanyamapori;

Dkt. Freddy Manongi        - Mhifadhi Mkuu, Mamlaka ya Hifadhi ya
                                           Ngorogoro; 

Bw. Allan Kijazi                - Mkurugenzi Mkuu, Hifadhi za Taifa;
Mwenyekiti, Muungano wa Jumuiya Zilizoidhinishwa;
Wakurugenzi/ Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali
(USAID, WWF, FZS, AWF, WCS);
Viongozi wa Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori;
Wawakilishi kutoka Sekta binafsi;
Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii;
Maafisa Wanyamapori wa Wilaya;
Mabibi na Mabwana.

Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote katika mkutano huu muhimu unaolenga kutathmini ustawi na changamoto zilizojitokeza/zinazojitokeza katika usimamizi wa shughuli za uhifadhi kwenye Maeneo ya Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori “Wildlife Management Areas” (WMAs) nchini.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana  
Sera ya wanyamapori ya mwaka 1998 kwa mara ya kwanza nchini ilielekeza kuanzisha dhana ya ushirikishaji wa jamii katika uhifadhi wa wanyamapori. Dhana hii inatoa fursa kwa wananchi kushiriki katika uhifadhi kwa kutenga maeneo ya ardhi ya vijiji ili kusimamia na kunufaika moja kwa moja kupitia rasilimali ya wanyamapori. Utekelezaji wa dhana hii ulianza rasmi mwaka 2003 na hadi sasa maeneo ya WMAs 21 zenye ukubwa wa kilometa za mraba 36237.7 yameidhinishwa na kutangazwa katika gazeti la serikali. Aidha, maeneo mengine 17 ya WMA yapo katika hatua mbalimbali za uanzishwaji.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana 
Kwa miaka 12 ya utekelezaji wa dhana hii tumeshuhudia mwamko katika jamii kushiriki katika kiuhifadhi, na wao kujipatia manufaa ikiwemo ajira, kipato katika ngazi ya jumuia, vijiji husika na kuchangia katika miradi ya maendeleo katika sekta za elimu, afya, maji. Pamoja na mafanikio haya bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji wa dhana hii nchini. Hivyo mkutano huu ni mwendelezo wa matokeo ya tuliyojifunza wakati wa kutekeleza dhana ya kushirikisha jamii katika uhifadhi kwa kuwaleta pamoja wadau muhimu na wataalamu ili kubadilishana uelewa, uzoefu, matokeo ya tafiti, na kutoa fursa ya mjadiliano rasmi yenye malengo kujitathimini mahali tulipotoka, tulipo na  tunapotakiwa kwenda.

Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana 
Naomba nijikite katika changamoto chache lakini muhimu ambazo mimi kama Waziri mwenye dhamana nimeziona katika kutekeleza majukumu yangu ambayo ningependa kupitia mkutano huu uziangalie kwa kina na kutusaidia kutoa ushauri wa kuandaa maelekezo ya kisera yatakayoweza kutoa majibu kama ifuatavyo:
1.   Kuchangia uboreshaji wa utawala bora katika rasilimali za wanyamapori na matokeo ya jamii na uhifadhi wa wanyamapori, ikiwa pamoja na kuhakikisha utawala bora kulingana na maslahi na haki za jamii (muingiliano wa mamlaka kati ya viongozi wa wilaya, vijiji na wale wa jumuiya/WMA na mgongano wa maslahi).
2.   Migogoro inayotokana na uwekezaji katika maeneo ya WMA mfano MBOMIPA.
3.   Mgogoro unaotokana na gharama za watalii katika hoteli na loji zilizopo ndani ya hifadhi za Taifa na zile zilizopo ndani ya WMAs zinazopakana.
4.   Uwiano wa mgawanyo wa mafao yatokanayo na uwekezaji katika maeneo ya WMAs kati ya Jumuiya/WMA, Serikali kuu, halmashauri za wilaya na vijiji wanachama.
5.   Matumizi ya fedha/mapato zinazotokana katika WMA na katika vijiji kutofanya kazi zitarajiwa.
6.   Ucheleweshaji wa mgao wa fedha unaotakiwa kupelekwa katika WMAs kutoka Serikalini.

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana, 
Mkutano huu ambao ni wa kwanza kufanyika na kukutanisha Wizara, Jumuiya Zilizoidhinishwa na Wawezeshaji wa WMAs ni fursa muhimu ambayo ikitumika ipasavyo na kwa nia njema itatoa suluhisho lkwa changamoto nilizozianisha hajo juu. Hivyo natoa wito kwa washiriki wa mkutano huu kuhakikisha fursa hii haipote bali itoe tija katika ustawi wa dhana ya kushirikisha jamii katika uhifadhi endelevu na wenye manufaa kwa jamii.

Wageni Waalikwa Mabibi na Mabwana 
Mwisho lakini sio kwa umuhimu napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wawezeshaji katika uanzishaji na uendeshaji wa WMA. Kipekee nitambue michango iliyotolewa na  USAID, WWF, FZS, AWF, WCS, KfW, BTC, DANIDA, GTZ (GIZ) na AFRICARE. Aidha, ninawashukuru USAID, AWF na WWF kwa ufadhili wao katika kufanikisha mkutano huu. Ni matumaini yangu kuwa mkutano huu utaleta tija inayokusudiwa ili kuhakikisha kuwa shughuli za uhifadhi katika WMA zinaendeshwa kwa ufanisi.

Natangaza rasmi Mkutano huu umefunguliwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad