HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 31, 2015

UMOJA WA MATAIFA WAPITISHA KWA KAULI MOJA AZIMIO DHIDI YA UJANGILI WA WANYAMAPOLI

Kifaru ni baadhi ya wanyamapori wanaotoweka kwa kasi duniani na hususani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kutokana na vitendo vya ujangili na biashara haramu za pembe zao. Jana Alhamisi Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja Azimio linalolenga kudhibiti Biashara haramu ya wanyama pori na maliasili nyingine

Na Mwandishi Maalum, New York

Kwa mara ya kwanza jana alhamisi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limepitisha kwa kauli moja, azimio la kihistoria linalolenga pamoja na mambo ya mengine kuitaka jumuiya ya kimataifa kushirikiana kwa karibu katika kuvikabili vitendo vya ujangili na biashara haramu ya wanyapori na maliasili nyingine. Aidha azimio hilo linamtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuteua mjumbe maalum atakayesimamia suala hilo pamoja na kutoa taarifa ya utekelezaji wa azimio hilo.

Azimio hilo linazitaka nchi mbalimbali kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kulichukulia kama ni kosa kubwa kwa mujibu wa sheria za nchi hizo Azimio hilo limeandaliwa na kundi la nchi marafiki dhidi ya ujangili na biashara haramu ya wanyapori. Kundi hilo ambalo Tanzania kupitia Uwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa, ni sehemu ya kundi marafiki liko chini ya uenyekiti weza wa Ujerumani na Gabon.

Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ulishiriki kikamilifu katika hatua zote za maandalizi na majadiliano yaliyopelekea kupatikana kwa azimio hilo ikiwa ni pamoja na kuliunga mkono. Mataifa zaidi ya 70 zikiwamo Marekani, Uingereza , China Ufaransa, Japan, yameunga mkono azimio hilo ambalo linaelezwa kuwa linafungua ukurasa mpya katika harakati za kuwanusuru wanyamapori ambao ndio urithi wa dunia na wanaotoweka kwa kasi.

Azimio hilo lilopewa namba A/69/L.80 liliwasilishwa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Waziri wa Mambo ya Nje ya Gabon Bw. Emmanuel Issoze-Ngondet

Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, Bw. Harald Braun amezishukuru nchi zinazounda kundi la marafiki dhidi ya ujangili na biashara haramu ya wanyamapori kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha upatikanaji wa azimio hilo.

Akasema hakuna nchi yote iwayo duniani inayoweza yenyewe peke yake kuukabili ujangili na biashasa haramu ya wanyama pori, biashara ambayo amesema inathamani ya mabilioni ya dola za kimarekani na mtandao wake ni mkubwa na hatari.

“ Tunahitaji ushirikiano na nguvu za pamoja kuanzia kule ambako wanyama hawa wanauwa kwa sababu ya pembe zao, nchi ambako bidhaa hii haramu inapita au kusafirishwa na kule ambapo bidhaa hii inaishia” akasema Balozi wa Ujerumani. Akabainisha kwamba kila mwaka tembo zaidi ya mia huuawa kwasababu ya pembe zao na kutoa mfano kuwa kwamba mujibu wa takwimu  za serikali ya Tanzania, idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 60.
Tembo, moja ya urithi wa dunia, mnyama ambaye yumo hatarini kutoweka katika uso wa dunia kutoka na ujangili na biashara haramu ya pembe zake.

Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba A/69/L.80 linataka raslimali hii kulindwa kwa nguvu zote.

“ Wanyamapori wamo katika hatari kubwa hivi sasa kuliko wakati mwingine wowote, huu ni wakati wa vitendo ili kudhibiti athari za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira zinazosababishwa na ujangili na biashara haramu.

Naye msemaji wa Umoja wa Ulaya, pamoja na kuelezea kuwa kupitishwa kwa azimio hilo ni tukio la kihistoria, amesama EU itaendelea kutoa misaada yake katika eneo hilo la kuukabili ujangili na biashara haramu . Akazitaja Tanzania na Msumbiji kama miongoni mwa mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ambazo zinanufaika misaada ya EU katika eneo hilo.

Mwakilishi wa Uingereza pamoja na kuelezea namna gani serikali yake imekuwa mstari wa mbele katika kuukabili ujangili dhidi ya wanyamapori, amesema azimio hilo limepishwa siku chache baada ya Simba maarufu Cecil na kipenzi cha wengi kuuawa huko Zimbabwe, tukio ambalo limewagusa watu wengi na kulaaniwa vikali.

Na akasema kupitishwa kwa Azimio hilo kutasaidia sana katika kuwalinda wanyamapori na kwamba limepitishwa katika wakati muafaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad