HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 5, 2015

Tabora wafurahia huduma za madaktari Bingwa

Na Grace Michael, Tabora

WAGONJWA waliofika na kupata huduma za Madaktari Bingwa ambao wapo kwenye mpango unaoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wamefurahia huduma hizo na kusema kwamba zimeokoa fedha nyingi ambazo wangetakiwa kuzitumia kusafiri kufuata huduma hizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora, Kitete, walisema kwamba ujio wa Madaktari hao umewasaidia kupata huduma nzuri na zinazohitajika bila ya usumbufu wa aina yoyote na wala kutumia gharama kubwa.

“Kwa upande wangu nashukuru mno kwani nilifika hapa nikiwa na hali mbaya sana, nilikuwa siwezi hata kula wala kutembea, lakini nipofika na kuonwa na daktari Bingwa na kunipa huduma nina nafuu kubwa mno kwani naweza kula na kuzungumza vizuri,” alisema Bw. Shukuru Jumanne (33) Mkazi wa Ipuli mkoani Tabora.

Mgonjwa huyo alipata huduma ya kutolewa maji kwenye kuta za moyo ambayo yalikuwa yakimsabishia maumivu makali na kushindwa kupumua vizuri. Mgonjwa mwingine ambaye naye alipata huduma hiyo, Bi. Halima Juma (49) mkazi wa Ipuli, Tabora alisema kuwa ana faraja kubwa baada ya kupata huduma ya kutolewa maji ambapo sasa anaweza kupumua vizuri ikilinganishwa na mwanzo.

“Sikuwa na uwezo wa kufuata huduma hizi mbali hivyo ujio wa hawa wataalam kwangu ni kama muujiza, namshukuru sana Mungu kwa kuwaonesha NHIF mpango kama huu,” alisema Bi. Halima.

Mbali na wagonjwa hawa, pia ndugu wa wagonjwa ambao walikuwa na ndugu zao wakiwa kwenye chumba cha upasuaji, waliupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuona umuhimu wa kuleta wataalam hao mkoani Tabora. Walisema kuwa huduma kama za upasuaji na huduma zingine ambazo walitakiwa kuzifuata Muhimbili au Bugando wamezipata hospitalini hapa bila ya usumbufu wowote.

Wamesema kuwa kitendo cha madaktari bingwa kuja mkoani hapo kimewapunguzia gharama ambazo wangetakiwa kuzitumia, hivyo wameuomba Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuendelea na utaratibu huo ili kukomboa maisha ya Watanzania wengi wanaoishi katika mikoa ya pembezoni.

Mpaka sasa jumla ya wagonjwa 400 wameonwa na Madaktari Bingwa huku wagonjwa 25 wamefanyiwa upasuaji tangu zoezi hili lilipoanza siku ya Jumatatu.
Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wakihakikiwa nyaraka zao kabla ya kuingia kupata huduma za Madaktari Bingwa.
Wahitaji wa huduma za kitaalam wakisubiri kuwaona madaktari bingwa.
Baadhi ya ndugu wa wagonjwa na wagonjwa wakisubiri kumuona daktari Bingwa wa Masuala ya Moyo.
Dk. Peter Kisenge kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili akimjulia hali mgonjwa Shukuru Jumanne ambaye alimpa huduma ya kumtoa maji kwenye kuta za moyo.
Madaktari wakijiandaa kumhudumia Mgonjwa Halima Juma ambaye alikuwa na maji kwenye ukuta moyo.
Wananchi wakiwa na subira ya kukutana na wataalam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad