HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 4, 2015

Mradi wa Kinyerezi 1 kukamilika mwezi Juni,Wafikia asilimia 80 ya ukamilishwaji wake

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Meneja Miradi ya Kinyerezi Mhandisi  Simon Jilima amesema kuwa  mtambo wa Kinyerezi 1 unaojengwa na kampuni ya Yakobsen Elektro ya Norway  unatarajia  kukamilika mapema  Juni mwaka huu.

Mhandisi  Jilima aliyasema hayo mbele ya  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini  iliyofanya ziara katika mtambo  huo  ili kujionea maendeleo ya ujenzi wake. Kamati hiyo imeanza ziara  ya kutembelea miradi ya umeme iliyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida,  Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini aina  ya  tanzanite katika mkoa wa Manyara.

Mhandisi Jilima alisema kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia  80 na kufafanua  kazi inayofanyika kwa sasa ni kumalizia utandazaji wa nyaya, ufungaji wa mabomba  ya maji na  gesi  pamoja na ujenzi wa barabara za ndani.
Alisema kuwa ofisi kwa ajili ya watumishi   pamoja na  karakana kwa ajili ya kuhifadhia  mitambo imekamilika.
Akielezea gharama za mradi huo  Mhandisi  Jilima alisema  mpaka sasa serikali imelipa kiasi  cha Dola za Marekani milioni 167.2 na  kuongeza kuwa   kiasi cha  Dola za Marekani milioni 15 kinatarajiwa kumaliziwa kabla ya kukamilika kwa mradi.

Akielezea   changamoto katika utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi  Jilima alieleza kuwa awali changamoto kubwa ilikuwa ni  ukamilishwaji wa mradi   wa bomba  la  gesi  ili waweze kutumia  gesi  hiyo katika kuzalisha umeme lakini kutokana na kasi  ya mradi huo kuwa  ya kuridhisha wana imani kuwa  gesi itaanza kuzalishwa mapema  kabla ya kukamilika kwa mtambo wa Kinyerezi 1

“ Ndugu wajumbe, awali tulikuwa na wasiwasi wa kupatikana kwa gesi  kwa ajili ya kuzalisha umeme kupitia mradi wa Kinyerezi 1 kutokana na mradi wa  bomba la  gesi kuwa na changamoto nyingi, lakini baada ya kuona  mradi wa bomba la gesi uko katika hatua nzuri yaani zaidi ya asilimia 90, tunaamini kuwa  mara mtambo utapokamilika, gesi itakuwa imekwishaanza kuzalishwa na hapo ndipo tutaanza kuzalisha  umeme mara moja,” alieleza Mhandisi  Jilima

Akielezea fidia kwa wakazi waliopisha ujenzi wa mradi huo, Mhandisi  Jilima alieleza kuwa mradi wa Kinyerezi I ulikwishafanya tahmini  pamoja na kulipa fidia kwa wakazi waliopisha ujenzi wa mtambo huo tangu mwaka juzi.

Wakati huohuo wajumbe wa Kamati ya  Bunge ya Nishati na Madini  walipongeza hatua iliyofikiwa ya  ujenzi wa mtambo  huo  na kuitaka serikali kukamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 15 ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini), Charles Kitwanga (kulia) akimsikiliza kwa makini Meneja Mradi Mkazi wa Kampuni ya Yakobsen Elektro ya Norway inayojenga mtambo wa Kinyerezi I Markkli Repo ( wa pili kutoka kushoto) mara baada ya kuwasili katika eneo la mtambo huo ili aweze kuwaongoza wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenye ziara katika mitambo hiyo.
Meneja Miradi ya Kinyerezi Mhandisi Simon Jilima (kulia) akielezea maendeleo ya ujezi wa mtambo wa Kinyerezi I mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini), Charles Kitwanga (wa tano kutoka kulia), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Mbunge wa Lulindi- Masasi, Jerome Bwanausi (katikati) akisisitiza jambo katika ziara hiyo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Madini), Charles Kitwanga na kulia ni Meneja Miradi ya Kinyerezi Mhandisi Simon Jilima.
Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Mhandisi Felchesmi Mramba akielezea mikakati ya shirika la Tanesco kuboresha huduma za umeme nchini kote.

Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Wanja Mtawazo ( kulia) akisalimiana na Mbunge wa Lulindi- Masasi, Jerome  Bwanausi ( kushoto) ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mara baada ya kamati hiyo kuwasili katika eneo la mtambo wa kufua umeme wa Kinyerezi I. Kamati hiyo inafanya ziara katika miradi ya umeme katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini ya tanzanite katika mkoa wa Manyara ili kujionea maendeleo ya sekta hizo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad