HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, February 1, 2015

BASATA YAANZISHA MFUMO WA KUHIFADHI TAARIFA ZA KUMBI ZA BURUDANI

Mtaalam wa TEHAMA kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw. Rajab Sollo akiwaonesha watendaji wa Baraza hilo (Hawako pichani) kuhusu namna mfumo wa kanzidata ya kuhifadhi kumbi za Starehe na Burudani unavyofanya kazi kwenye mafunzo ya siku mbili yaliyofanyika mwishoni mwa wiki hii makao ya BASATA yaliyo Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Mtaalam wa IT kutoka BASATA Bwana Sollo (anayeonekana kwa mbele) akitoa mafunzo kwa watendaji wa BASATA kuhusu kanzidata ya kuhifadhi kumbi za Starehe na urudani nchini.
Sehemu ya watendaji waliohudhuria mafunzo hayo wakimfuatilia kwa makini Mkufunzi wa TEHAMA kutoka BASATA Bw. Rajab Sollo.

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeanzisha kanzidata (database) ya kuhifadhi taarifa mbalimbali za kumbi za starehe na burudani nchini ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu sahihi katika sekta ya Sanaa nchini.

Akizungumza mwishoni mwa wiki hii wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya watendaji wa BASATA kuhusu matumizi sahihihi ya kanzidata hii yaliyofanyika ofisi za BASATA zilizoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza alisema kwamba kuanzishwa kwa kanzidata hiyo ni mwanzo wa kuhifadhi taarifa na takwimu zote zihusuzo sekta ya Sanaa.

“Tumeanza na kumbi za starehe na burudani zilizoko nchi nzima, lakini lengo ni kuweza kuhifadhi taarifa za wasanii wote nchini, mapromota, vyama vya wasanii na asasi mbalimbali zilizosajiliwa lakini pia kuwa na taarifa zote zihusuzo sekta ya Sanaa nchini” alisisitiza Mngereza.

Aliongeza kwamba, BASATA limezamilia kuhama kutoka mfumo wa kianalojia na kuanza kuhifadhi nyaraka na taarifa zake kidijitali na kwamba programu hii ya kujenga kanzidata itafanyika kwa awamu hadi itakapokamilika.

Awali akitoa mafunzo ya matumizi ya kanzidata hii, Mtaalam wa Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka BASATA Rajab Sollo alisema kwamba kanzidata hii ya kumbi itawezesha kupatikana kwa taarifa za kumbi za burudani zote nchini, umiliki wake, mawasiliano, picha na taarifa mbalimbali muhimu kwa utendaji.

Alisema kwamba, kanzidata hiyo imeandaliwa kwa ubora mkubwa ikiwa imezipanga kumbi kwa mikoa na wilaya zinakopatikana ambapo sasa itakuwa ni rahisi kuweza kujua idadi sahihi ya kumbi zilizosajiliwa, zilizo na vibali na zile ambazo hazijakamilisha taratibu za vibali.

Pia alisema kwamba baada ya kukamilika kwa kanzidata ya kumbi, BASATA itaanza kuandaa kanzidata ya wasanii na wadau wote wa Sanaa nchini ambapo hadi itakapokamilika taarifa zote zihusuzo sekta ya Sanaa nchini zitakuwa zikipatikana kwa urahisi na haraka mtandaoni.

“Tumezamilia kuhifadhi taarifa zote za sekta ya Sanaa na kuzifanya zipatikane kiurahisi. Kazi kubwa inahitajika na tumejipanga kukamilisha zoezi hili mapema iwezekanavyo” alisisitiza Sollo.

Katika siku za karibuni baadhi ya wasanii na wadau wa Sanaa wamekuwa wakitoa maneno yanayolinasabisha BASATA na uzee hali ambayo ni tofauti uhalisia na kuzinduliwa kwa kanzidata hii ni hatua kubwa katika mabadiliko ya mifumo ya kiutendaji ndani ya Baraza hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad