HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 27, 2015

TTCL na Huawei waingia mkataba wa kuboresha mawasiliano nchini

Afisa Mtendaji Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL),Kamugisha Kazaura (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa MS Huawei Technologies,Bruce Zhang wakisaini mikataba ya makubaliano ya kupanua na kuboresha mtandao wa TTCL wa simu za mezani, mkononi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao unagharimu zaidi ya kiasi cha dola za kimarekani Milioni 182.
Afisa Mtendaji Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL),Kamugisha Kazaura (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa MS Huawei Technologies,Bruce Zhang wakibadilishana mikataba ya makubaliano ya kupanua na kuboresha mtandao wa TTCL wa simu za mezani, mkononi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao unagharimu zaidi ya kiasi cha dola za kimarekani Milioni 182.
Picha ya Pamoja.

Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL)  na Kampuni ya MS Huawei Technologies ya China wameingia mkataba utakaolenga katika kujenga, kupanua na kuboresha mtandao wa TTCL wa simu za mezani, mkononi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo miradi hiyo itagharimu zaidi ya kiasi cha dola za kimarekani Milioni 182.

Awamu ya kwanza ya mradi huu inategemea kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, 2015.

Miradi ambayo iko kwenye mkataba itahusisha ujenzi wa mtandao wa teknolojia ya kisasa ya 4G Long Term Evolution (LTE), 3G - UMTS pamoja na 2G- GSM, teknolojia hizi zitasaidia Kampuni kupanua na kuboresha huduma zake nchi nzima na katika ubora wa hali ya juu. Teknolojia hizi zitatoa huduma bora ya sauti na intaneti (data) yenye kasi zaidi.

Mkataba huu pia unahusisha ununuzi wa mitambo kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini chini ya mpango wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF).

TTCL imeshinda zabuni ya kupeleka mawasiliano katika kata 69 zinazojumuisha vijiji zaidi ya 400 vyenye wakaazi zaidi ya laki tano. Chini ya mradi huo UCSAF itaipatia TTCL Dola za Marekani milioni kumi kujenga miundo mbinu ya mawasiliano katika Kata hizo.

Mkataba wa TTCL na Huawei ni moja ya juhudi zinazofanywa na Kampuni katika kutekeleza mikakati endelevu ili kuboresha na kupanua upatikanaji wa huduma nafuu za mawasiliano ya simu na intaneti nchi nzima.

Aidha, mikakati hii inaunga mkono juhudi za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha huduma za simu na intaneti zinawafikia watanzania waliopo vijijini na mjini.

Hivyo, TTCL inawahakikisha watanzania na wateja wake wote kuwa iko imara, na imejipanga kimkakati katika kuhakikisha inaendelea kutoa huduma endelevu, bora na nafuu kwa wateja wetu wa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

1 comment:

  1. well done, but you have to prove to us that you are capable to deliver the best services ......... we are keeping our eyes open.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad