HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 26, 2014

OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU KUADHIMISHA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA KESHO

Na Veronica Kazimoto - MAELEZO

Tanzania itaungana na nchi nyingine barani Afrika katika kuadhimisha Siku ya Takwimu Afrika ambayo itafanyika tarehe 27 Novemba, 2014 katika ukumbi wa mikutano uliopo Jumba la Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ephraim Kwesigabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema lengo la kuadhimisha siku hiyo ni kuongeza ufahamu kuhusu nafasi na mchango wa tasnia ya takwimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika.

Kwesigabo amesema kuwa, Kaulimbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka 2014 ni “Takwimu Huria kwa Uwajibikaji na Ushirikishwaji wa Wadau wote”.

“Kaulimbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka huu imebeba ujumbe muafaka ambapo kwa kuwa sasa maendeleo ya Afrika yanategemea takwimu huria katika kuongeza uwajibikaji na ushirikishwaji katika kuandaa sera, kupanga na kutathmini mipango mbalimbali ya maendeleo na kufanya maamuzi sahihi, amefafanua Kwesigabo”.

Takwimu huria ni takwimu na taarifa zinazozalishwa kwa ubora na viwango   kutokana na tafiti au taarifa za kiutawala ambazo zinatolewa, kusambazwa na kutumiwa na mtu yeyote bila kikwazo chochote.

Akielezea baadhi ya sifa za takwimu huria Mkurugenzi Kwesigabo amesema ni pamoja na upatikanaji wake kwa urahisi kulingana na mahitaji ya watumiaji, ziwe kamilifu kwa kutoa ujumbe sahihi na unaoeleweka na ziwe katika mfumo utakaomrahisishia mtumiaji kuzitumia kulingana na mahitaji yake pasipo kizuizi chochote.

Sifa nyingine za takwimu huria ni kutokuwa na ubaguzi, zitolewe kwa wakati, na muundo wa uhifadhi wake uwe rahisi ambao unaweza kusomeka katika programu mbalimbali za kompyuta.

Kwesigabo ameongeza kuwa Serikali ya nchi yoyote inapokuwa na mfumo wa takwimu huria, huwezesha wananchi na wadau wengine kupata taarifa na takwimu zinazozalishwa katika nchi hiyo bila kizuizi chochote. Aidha, huongeza uwazi na ushirikishwaji wa wananchi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.

Washiriki mbalimbaliwa kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Vyuo vya Elimu ya Juu, Wanafunzi wa Shule za Sekondari pamoja na Wadau wengine wa takwimu nchini wanatarajia kuhudhuria katika maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika hufanyika tarehe 18 Novemba, kila mwaka lakini kwa Tanzania maadhimisho hayo yatafanyika kesho tarehe 27 Novemba, 2014.
Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephrahim Kwesigabo, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu Siku ya Takwimu Afrika itakayo adhimishwa Dar es Salaam kesho. Kulia ni Mtakwimu Mkuu, Adella Ndesengia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad