HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, August 23, 2014

JESHI LA POLISI MKOANI PWANI LAWATIA MBARONI WA ETHIOPIA 48 WALIOINGIA NCHINI KWA MLANGO WA UWANI

Na John Gagarini, Kibaha

JESHI la Polisi mkoani Pwani linawashikilia raia 48 wa nchi ya Ethiopia kwa tuhuma za kuingia nchini bila ya kibali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Kaimu kamanda wa Polisi mkoani humo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema kuwa watuhumiwa hao walitelekezwa vichakani.

Kamanda Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 21 mwaka huu majira ya saa 7 usiku katika Kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze wilayani Bagamoyo.

Alisema kuwa Wethiopia hao waligunduliwa na askari Magereza wa Gereza la Ubena aitwaye Sospeter ambaye aliwakuta porini alipokuwa akifanya shughuli zake na kutoa taarifa polisi.

"Kati yao 11 wanaumwa na wamepelekwa kituo cha afya cha Chalinze kwa ajili ya matibabu baada ya kuonekana wakitapika baada ya kupewa chakula na walionekana wakiwa na hali mbaya ya kiafya huku wale wengine wakiwa wamehifadhiwa kwenye kituo cha polisi cha kiwilaya," alisema Kamanda Mwambalaswa.

Aidha alisema kuwa raia hao wa Ethiopia wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 20 na 40 na wanatarajiwa kukabidhiwa idara ya Uhamiaji kwa ajili ya taratibu zingine ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazowakabili.

Wakati huo huo mtu mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya (25) na (28) amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia kamaba ya katani.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 22 mwaka huu majira ya saa 2 usiku Kijiji cha Kibiki kata ya Bwiringu Tarafa ya Chalinze.

"Mfanyakazi wa shambani wa mwenyekiti wa Kijiji hicho alimpa taarifa bosi wake aitwaye Ally Hussein (47) kuwa kuna mtu kajinyonga kwenye banda lake ambaye naye alitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo," alisema kamanada Mwambalaswa.

Aliongeza kuwa marehemu aliacha ujumbe amabo uliandikwa kwenye karatasi kuwa anawaachia dunia ili waishi miaka 120, hakuna mtu aliyekamatwa na polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad