HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 21, 2014

DK. KAMANI ATEMA CHECHE BUSEGA

NA MWANDISHI WETU, BUSEGA
 
MWENYEKITI wa CCM mkoani Simiyu, Dk. Titus Kamani, amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo Madiwani, Makatibu wa Chama na Jumuia zake, kujiwekea ratiba ya kutembelea wananchi ili watambue kero zinazowakabili.

Dk. Kamani, ambaye pia ni Mbunge wa Busega na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na baadhi ya viongozi wa Chama katika Kijiji cha Lamadi wilayani Busega.

Alisema huu sio wakati wa kukaa na kubweteka ofisini kusubiri wananchi wapelekea kero, bali ni wakati wa kuwatembelea na kufanya mikutano na kuwajulisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya maendeleo ambayo yanatekelezwa kutokana na Ilani ya CCM.

“Madiwani wenzangu, wenyeviti, makatibu wa Chama na jumuia zetu ikiwemo ya vijana, msiwasahau wananchi, jiwekeeni utaratibu wa kuwatembelea ili mfahamu kero zao, msidhani mikutano ya mbunge pekee ndiyo njia ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi,” alisema.

Aliwataka viongozi hao kamwe wasibweteke wala kusuasua katika kufanya mikutano na kutembelea wananchi, ambao kimsingi ndio wanaowatumikia.

“Ndiyo maana tumewapa baiskeli makatibu watendaji wa Chama na UVCCM wa kila Kata ili ziwasaidie kuwafikia wananchi na wanachama kwa wakati muafaka, nao wana wajibu wa kuwatembelea wananchi na kukiimarisha Chama,” alisema Dk. Kamani.

Hivi karibuni, Mwenyekiti huyo wa Chama wa mkoa wa Simiyu alitoa baiskeli 39 zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 5.8 kwa wenyeviti na makatibu Kata wa CCM na Makatibu wa UVCCM kwa ajili ya kuwasaidia usafiri wa kuwafikia wanachama na wananchi kwa urahisi.

Awali, mwishoni mwa wiki, Dk Kamani alitembelea na kukagua ujenzi wa wodi ya Wazazi unaendelea katika Zahanati ya Kata ya Lamadi Kijijini Lukungu, inayojengwa kwa thamani ya sh. milioni 75 zilizotolewa na AMREF mkoani Simiyu, chini ya kampeni ya Uzazi-Uzima.
Mbunge wa Jimbo la Busega, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, akishuhudia maji yakitiririka baada ya kukamilika kwa mradi wa maji wa Kijiji cha Manala Kata ya Badugu wilayani Busega. Kulia ni Katibu wa CCM wa Wilaya ya Busega, Agatha Magonela.
 Dk. Titus Kamani, akimtwisha ndoo ya maji mama mmoja mkazi wa Kijiji cha Manala, baada ya kufungua mradi huo.
 Dk. Kamani akikagua msingi wa Kituo cha kulelea walemavu wa ngozi (albino) kinachojegwa katika Kijiji cha Lukungu Lamadi wilayani humo, mbele yake ni Mratibu wa kituo hicho, Mudy Gimonge.
 Dk. Kamani akishiriki na baadhi ya wananchi wa Lukungu kusomba tofali za ujenzi wa kituo cha kulelea walemavu wa ngozi (albino).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad