HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 19, 2014

Mechi ya Simba na Yanga yaelimisha namna ya kupambana na Malaria

Kampuni ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana Taasisi ya Malaria No More na THT(Tanzania house of talent) leo wameitangaza rasmi nambari maalum ambayo wateja wanaotumia huduma za Vodacom wanaweza kuitumia kupata taarifa zinazohusiana na ugonjwa wa malaria.

Ili mteja kuweza kupata taarifa hizo zinazohusisha jinsi ya kujikinga, tiba na masuala mengine mbalimbali ya Malaria anachopaswa mteja kufanya ni kujiunga kwa kutuma neno "Malaria" au "Mzinduka" kwenda nambari 15760 bila malipo.

Ujio wa huduma hii ni sehemu ya kampeni kabambe ya Mzinduka inayolenga kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria hapa nchini ambayo Vodacom Foundation ni mshirika wake.

Nambari hiyo imetangazwa jijini dar es salaam kwenye uwanja wa taifa muda mfupi kabla ya kuanza kwa mechi kati ya Simba na Yanga kwa lengo la kuwashirikisha washabiki wa soka nchini kuunga mkono kampeni hiyo.

"Ni imani yetu kuwa kupitia huduma hii wananchi watakuwa na fursa rahisi na nyepesi ya kujua mambo mbalimbali yanayohusu malaria na ni kwa njia hiyo tunaweza kuishinda vita dhidi ya ugonjwa huo hatari unaoongoza kwa kusababisha vifo ikiwemo wanaawake wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano"alisema Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom Salum Mwalim

Amesema kampuni ya Vodacom kupitia mfuko wake wa kusaidia jamii wa Vodacom Foundation imeona umuhimu wa kuunga mkono kampeni hiyo kutokana na ukweli kwamba ugonjwa wa malaria ni tishio na kwamba maisha ya watu lazima yalindwe.

"Kupitia Vodacom Foundation, Tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuunganisha watu na kuyabadili maisha yao kupitia teknolojia ya simu za mkononi na sasa tunataka tuitumie teknolojia hiyo ya simu za mkononi kuokoa maisha yao, hii ni njia rahisi na isiyo na gharama kwa mteja wetu."Aliongeza Mwalim

Amesema wameutumia mchezo wa Simba na Yanga kutangaza nambari hiyo ikitambua ukubwa wa mtandao wa washabiki wa mpira wa miguu nchini ambao ukitumika vema ni wazi utatoa mchango mkubwa katika kuipatia kampeni hiyo ufanisi.

"Tunataka ujumbe huu ufike kwa kila mtanzania ili kwa pamoja tuweze kuhakikisha kila mmoja wetu ana taarifa sahihi za malaria na hivyo kulinda maisha yake na ya wanaomzunguka,kupitia michezo hususan soka hilo linawezekana kwa wepesi na haraka zaidi"

Kwa muda wa miaka 10 sasa iliyopita Tanzania imekuwa  kati ya nchi zilizokuwa kwenye mstari mbele kupigana na ugonjwa huu wa malaria na vimepungua kwa asilimia 50. 

Kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya Malaria No More Lilian Madeje ametoa rai kwa watanzania kuitumia huduma hiyo ili kupunguza pengo la upatiakanaji wa taarifa sahihi zinazohusu Malaria

"Pamoja na kuwepo na changamoto nyengine kadhaa katika vita dhidi ya malaria bado suala la wananchi kuwa na taarifa sahihi za malaria ni jambo la muhimu ili kumuwezesha kila mmoja kutambua namna ya kujikinga, kugundua viashiria ama dalili za ugonjwa wa malaria na namna ya kupata tiba bora na iliyo sahihi."

Amesema mara mteja anapojiunga atakuwa akipokea taarifa mbalimbali bila ya gharama yoyote na mutoa rai kwa kila mmoja kuwa balozi kwa mwenzake katika kuhamamisha matumizi ya huduma hiyo.

Huduma hiyo ni sehemu ya kampeni ya Mzinduka iliyozinduliwa na Makamunwa rais Dk Mohamed Gharib Bilala Disemba mwaka jana.

Chini ya kampeni hiyo, njia mbalimbali zenye mvuto kwa makundi kadhaa hususan vijana zinatumika katika kueneza ujumbe wa malaria na kuishajihisha jamii kuunga mkono vita dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad