HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 23, 2014

JIJI LA DAR ES SALAAM KUENDELEA KUSAFISHWA - MKUU WA MKOA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki akitoa taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) ofisini kwake leo jijini Dar es salaam. 

Na. Aron Msigwa –MAELEZO,Dar es salaam.

Jumla ya kata 22 katika manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke zitaingizwa katika  mpango wa utengaji wa maeneo maalum (smart area) kwa ajili ya kuboresha usafi wa mazingira jijini Dar es salaam.

Akitoa taarifa ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Dar es salaam (RCC) leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema uanzishaji wa maeneo maalum ya usafi wa mazingira unalenga kuondoa shughuli zote zinazofanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji kinyume  cha sheria na  kulifanya jiji la Dar es salaam kuendelea kuwa katika hali isiyoridhisha ya usafi wa mazingira.

Amesema utekelezaji wa mpango huo wa utengaji wa maeneo maalum unazingatia sheria ya mipango miji Na. 8 ya mwaka 2007 na sheria ya mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 na kuzitaja kata  zitakazohusika katika mpango huo kuwa ni pamoja Keko, Chang’ombe, Kurasini, Mibulani , Sandali na kata ya Gerezani zote za manispaa ya Temeke.

Kata nyingine ni Mchafukoge, Kariakoo, Mchikichini, Jangwani, Kisutu, Kivukoni,Upanga Mashariki na Upanga Magharibi ambazo ziko manispaa ya Ilala na kata za Hananasif, Kinondoni, Kigogo, Mzimuni na Magomeni zote za manispaa ya Kinondoni.


Amesema kuwa ili kufanikisha  utekelezaji wa mpango huo hatua mbalimbali zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuondoa shughuli zote zinazosababisha kero katika eneo husika, biashara zisizo rasmi, biashara za vyakula, uchomaji nyama na mahindi kando kando ya barabara na maeneo ya watembea kwa miguu, uondoaji wa gereji bubu, maguta, mikokoteni bajaji na bodaboda katikati ya jiji.

Shughuli nyingine zitakazofanyika ni zile za uondoaji wa malori makubwa yenye zaidi ya tani 10 katika maeneo yasiyoruhusiwa na kubainisha halmashauri zinaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli hizo.

“Halmashauri zetu zinaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli zote tulizoziainisha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi japo kuna maeneo tuliyoyatenga kwa wananchi hayatumiki na baadhi ya wahusika hawako tayari kwenda kwenye maeneo hayo”  amesema.

Kuhusu waendesha bodaboda na bajaji kuendelea kuingia katika maeneo yasiyoruhusiwa hususani katikati ya jiji la Dar es salaam amesema kuwa serikali haitalifumbia macho suala hilo kwa kuwa liko kisheria.

Amesema watekelezaji wa sheria ya SUMATRA ya kuhifadhi maeneo yaliyotengwa wanaendelea na zoezi la kuwaondoa wote wanaovunja sheria hiyo na kutoa wito kwa wahusika wa zoezi hilo kuliendesha kwa kufuata sheria, taratibu na kuzingatia utu na haki za binadamu.

“Nimeshatoa maagizo kwa watendaji na viongozi wanaosimamia zoezi hili wahakikishe wanaheshimu utu na haki za binadamu, kama ni kampuni ikigundulika tutaifungia isipate tenda zozote za serikali, nachosema wahusika wawe makini serikali hatutawavumilia wanaoendesha vitendo vya hujuma, uonevu, wizi, uporaji na ukiukaji wa haki za binadamu” Amesisitiza.

Aidha ameeleza kuwa  mkoa wa Dar es salaa licha ya kukabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti unaendelea kutekeleza shughuli  mbalimbali  zenye tija kwa maendeleo ya wananchi zikiwemo Elimu, Afya, ujenzi na ukarabati wa barabara, madaraja na miundombinu mingine ya jiji ambayo imeharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema katika kuimarisha huduma za afya mkoa kupitia kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) imepitisha maombi maalum ya zaidi ya shilingi bilioni 45 nje ya bajeti ili kukabiliana na tatizo la msongamano mkubwa wa wagonjwa wa nje na wale wanaolazwa katika hospitali za mkoa wa Dar es salaam.

Amesema kuwa mkoa wake unapata wagonjwa wengi wa nje kutoka maeneo mbalimbali yakiwemo ya Kisarawe, Mkuranga, Mafia, wilaya ya Bagamoyo,Kibaha na Chalinze jambo linaloongeza mzigo kwa hospitali za mkoa huo.

“Mkoa wa wetu wa Dar es salaa una idadi kubwa ya watu kuliko mikoa mingine nchini pia unahudumia watu wengine wengi kutoka maeneo mbalimbali, jambo hili linaongeza mzigo kwa hospitali zetu kutokana na kuwahudumia wananchi kutoka nje ya mkoa” Amesisitiza.

Ameeleza kuwa wagonjwa wa nje sasa wanafikia 1500 hadi 2000 kwa siku jambo linalowafanya kuomba fedha zaidi kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa hospitali za rufaa za mkoa na ujenzi wa hospitali maalum kwa ajili ya mama na motto itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 600 kwa wakati mmoja.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki ameeleza kuwa mkoa wake una dhamira ya kuongeza maeneo mapya ya utawala kwa kuongeza kata 113 na mitaa 570 pamoja na kupitia mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye kikao Maalum cha kamati ya ushauri ya mkoa na  mabaraza ya madiwani  ya halmashauri husika kuhusu  kuugawa mkoa wa Dar es salaam katika muundo wa wilaya 5.

Amesema kuwa wilaya zilizopendekezwa ni pamoja na Ilala, Kinondoni, Temeke, wilaya ya Kigamboni na wilaya ya Ubungo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad