HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 10, 2013

Norway yaisaidia Tanzania Sh. bilioni 200 kwa ajili ya umeme vijijini

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (kushoto), akiwa na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Bw. Heikki Holmas, muda mfupi kabla ya kusaini Mkataba wa Krona 700 (sawa na sh. bilioni 200 za Tanzania) uliotolewa na Serikali ya Norway kwa Watanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini.
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (kushoto), akitiliana saini na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Bw. Heikki Holmas kuhusu msaada wa Krona 700 (sawa na sh. Bilioni 200 za kitanzania) kutoka Serikali ya Norway kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini.
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (kushoto), akipeana mkono na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Bw. Heikki Holmas, baada ya kusaini mkataba wa Krona 700 (sawa na sh. Bilioni 200 za Tanzania) uliotolewa na Serikali ya Norway kwa Watanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini.

Serikali ya Tanzania imekamilisha makubaliano ya fedha za msaada wa Krona 700, sawa na shilingi bilioni 200 za Tanzania, kutoka Serikali ya Norway, kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo alisaini mkataba wenye makubaliano hayo jana, Aprili 9, 2013 Mjini Oslo Norway akiiwakilisha Serikali ya Tanzania, ambapo Serikali ya Norway iliwakilishwa na Waziri wake wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa, Bw. Heikki Holmas.

Zoezi la kusaini mkataba huo lilifanyika mwishoni mwa Mkutano ambao Waziri Muhongo alishiriki uliobeba dhima isemayo ‘Nishati na Maendeleo Kuanzia 2015’. Malengo mahsusi ya mkutano yalikuwa ni kufanya majumuisho ya majadiliano mbalimbali kuhusu nishati ambayo yamekuwa yakifanyika ulimwenguni kote na katika mitandao, na pia kutoa mapendekezo kuhusu nafasi ya nishati katika maendeleo kuanzia mwaka 2015.

Akizungumzia msaada huo, Prof. Muhongo alisema “sasa tunao uhakika wa kumaliza miradi ya umeme kwenye Wilaya mpya 13, zoezi litakalogharimu takribani shilingi bilioni 70 za kitanzania, na pia kukamilisha miradi mingine ya umeme vijijini.”

Kwa upande wake, Waziri Holmas alisema “kuwapatia watu waishio vijijini huduma ya umeme ni sawa na kuwapatia Watanzania wengi uwezekano wa kuondokana na matumizi ya nishati zenye uharibifu kama mafuta ya taa na dizeli.” Alifafanua kuwa msaada huo unalenga kuleta usawa kwa vitendo, ambao utainua hali ya maisha haraka na kuleta njia mbadala za kujipatia kipato kwa wananchi wa vijijini.

Alisema, zaidi ya asilimia 90 ya msaada uliotolewa itatumika kuweka umeme kwa kuongeza miundombinu ya usambazaji wa umeme, ambapo kwa mujibu wake ndiyo namna nzuri zaidi ya kuyafikia maeneo ya vijijini kwa huduma husika, kulingana na uzoefu.

Profesa Muhongo alisema Tanzania imedhamiria kuongeza huduma ya upatikanaji wa nishati ya umeme kwa Watanzania kutoka asilimia 18.4 hadi 30 kwa ngazi ya taifa, na kutoka asilimia 6.5 hadi 15 kwa maeneo ya vijijini.

Baada ya Mkutano na makubaliano hayo, Waziri Muhongo ameendelea na safari yake katika Mji wa Brussels, Ubelgiji akiendelea na zoezi la kutafuta fedha za miradi mbalimbali ya umeme.

2 comments:

  1. Brussels sio Ujerumani ni Belgiam

    ReplyDelete
  2. Samahani kaka, naomba fanya correction haiwezekani hizo Krona ziwe 700 ni sawa na TShs. 200 billion - cheki exchange rate.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad