HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 28, 2011

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL AKUTANA NA MABALOZI WA NCHI ZA SUDAN, KENYA NA ZAMBIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Zambia nchini Tanzania, Mavis Lengalenga, baada ya mazungumzo wakati alipomtembelea ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, John Mutinda Mutiso, wakati alipofika kumtembelea na kufanya mazungumzo ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Sudan Nchini Tanzania, Abdelbagi Hamdan Kabeir, wakati alipomtembelea ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo  na kufanya mazungumzo. Picha na Muhidin Sufiani - OMR 

Na. Boniphace Makene.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Jumanne Juni 28, 2011 ametembelewa na Mabalozi wa nchi tajwa hapo juu ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam. 


Ziara ya kwanza ilikuwa ya Balozi wa Sudan  Abdelbagi Hamdan Kabeir ambaye alifika kwa lengo la kumsalimia Makamu wa Rais huku pia akitumia fursa hiyo kumuaga kufuatia muda wake wa kushika wadhifa huo hapa nchini kufikia mwisho.


 Balozi Kabeir alifafanua kuwa maisha yake nchini Tanzania yamemfanya kuifahamu nchi yetu na anashukuru kwa ushirikiano wa wananchi wa Tanzania hali inayompa fursa sasa kuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini kwao.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Bilal alimshukuru Balozi Kabeir kwa kazi nzuri na hasa katika sekta ya elimu ambapo Watanzania kadhaa wamepata nafasi za kusoma nchini Sudan, huku pia nchi hiyo ikisaidia katika sekta ya elimu na kubadilishana wataalam wa sekta hiyo nchini. 

Pia Makamu wa Rais alifafanua kuwa, binafsi angependa kuona kura ya maoni iliyopigwa na kufanikisha kuundwa kwa nchi mpya Sudan Kusini inaheshimika na hivyo Sudan kuwa eneo la amani tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. 

Balozi Kabeir alimshukuru Makamu wa Rais na kisha kumuelezea kuwa wao kama Sudan wana mengi ya kujifunza katika kudumisha amani na akatumia mfano wa Zanzibar kama eneo ambalo Tanzania imeonyesha uwezo wake wa kumaliza kero za ndani kwa kutumia watu wa ndani kujadiliana na kukubaliana.

Kwa upande wa Balozi wa Kenya nchini; John Mutinda Mutiso yeye naye alitoa salamu za watu wa Kenya nchini kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana naye tangu achaguliwe katika wadhifa huo.

 Balozi Mutiso alimueleza Makamu wa Rais kuwa; Kenya inajifunza mengi kutoka Tanzania na akasifia namna Tanzania ilivyoendesha uchaguzi mkuu uliopita, huku akisema wao Kenya kila inapokaribia uchaguzi vidonda vyao vinaibuka na wananchi wanakuwa na hofu ya usalama wao wakati wa uchaguzi. 

Pia Balozi Mutiso alisifia kitendo cha Tanzania kutumia vyombo vya dola katika kuchunguza rushwa katika uchaguzi kwa kuanzia na kura za maoni katika vyama akasema jambo hili halifanyiki Kenya na wao wameona ni jema ambalo wangependa kuliiga.

Balozi Mutiso alimuomba Makamu wa Rais kukuza mashirikiano hasa katika eneo la Mazingira huku na akiielezea Tanzania kuwa iko juu katika utunzaji wa mazingira kulinganisha na Kenya na akamuomba Makamu wa Rais kama ataweza kuwa muda katika ratiba zake kuitembelea Kenya na kuhamasisha upandaji miti.

“Eneo kubwa ambalo Tanzania inaweza kutusaidia ni katika kupata miche ya miti. Tunahitaji kupanda miti kama milioni 100 na uwezo wetu wa kupata mbegu na miche ni mdogo kwa kuwa miti yetu mingi tumeitumia na sasa tunaumia,” alisema Balozi Mutiso.

Balozi huyo pia aliwataka Watanzania kuwa na subira na kuondoa jazba katika suala la kuandika Katiba mpya kwa kuwa wao Kenya iliwachukua miaka 20 hadi kupata katiba waliyonayo leo. “Zoezi hili ni gumu na linahitaji umakini. Hakuna watu kulitumia kwa sababu zao za kutafuta madaraka. Katiba ya nchi inapaswa kuwawakilisha watu wote na hasa walioko vijijini hivyo haiwezi kuandikwa kwa kukimbizana,” alisema Balozi Mutiso.

Makamu wa Rais alimshukuru Balozi wa Kenya na kumuahidi kufanya naye mazungumzo zaidi ya mashirikiano katika sekta ya mazingira hasa baada ya kikao hiki cha Bunge la Bajeti kumalizika.

Kwa upande wake Balozi wa Zambia nchini; Mavis Lengalenga Muyunda yeye alimshukuru Makamu wa Rais na wananchi wa Tanzania kwa ushirikiano wao katika kipindi hiki cha msiba wa kitaifa nchini Zambia, msiba wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Frederick Chiluba aliyezikwa jana. 

Balozi Muyunda alimuelezea Makamu wa Rais kuwa Zambia inathamini uhusiano wake na Tanzania na kwamba inaheshimu nafasi ya Tanzania katika utunzaji na uhifadhiji amani katika ukanda huu wa nchi za Kusini wa Afrika. 

Tena alifafanua kuwa kwa namna alivyofika Tanzania amebaini kuwa ni nchi yenye mikakati na akafafanua kuwa mfano wa kwanza ni bajeti ya mwaka huu ambayo inalenga kutoa majibu katika vipaumbele vinavyowagusa wananchi.

Kuhusu vyombo vya kiuchumi vinavyounganisha Tanzania na Zambia kama TAZARA, TAZAMA NA MOFET, Balozi Muyunda alisema nchi yake inaendelea na jitihada za kuiboresha TAZARA ambapo huko wameshapata mkopo toka China wenye lengo la kuboresha chombo hicho muhimu kwa usafirishaji wa ukanda wa Kusini.

Kwa upande wa Makamu wa Rais alimtakia kila la heri Balozi Muyunda hasa sasa ambapo Zambia inaingia katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Septemba ama mwanzoni mwa Oktoba. 

Pia alimsisitizia kuhusu umuhimu wa nchi hizi kuheshimu mambo mazuri waliyoyaanzisha waasisi wa nchi zetu mbili na kuhakikisha kuwa wanayafunza kwa vizazi vijavyo vya nchi hizi ili kuzidisha moyo wa kuthaminiana na kupendana kwa nchi zote mbili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad