HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 22, 2011

wasanii wa five star waliopata ajali na kufariki na wale waliojeruhiwa watajwa

Hili ndilo Lori lililokuwa limebeba mbao ambalo ndilo lililosababisha ajali iliyopelekea kupoteza maisha kwa wasanii 13 wa kikundi cha Taarab cha Five Star.
Baadhi ya wasamalia wema waliokuwa kwenye foleni ya magari baada ya kutokea kwa ajili ya Basi ndogo la Wasanii wa Kundi la Five Stars Moden Taarab wakichunguza kwa makini iwapo kuna mtu aliyebanwa ama kusahauliwa kuokolewa ama miili wake kubakia eneo hilo baada ya basi hilo kuparamia lori lililosheheni mbao lililokuwa limeharibika njiani , katika barabara kuu ya Iringa- Morogoro , eneo la Hifadhi ya Taifa ya wanyama ya Mikumi, karibu na Kijiji cha Doma, Wilaya ya Mvomero usiku wa kuamkia leo.
Lori lililoparamiana na basi la wanamuziki wa Five Stars

Msanii wa kikundi cha Taarab cha East African Melody Bi Mwanahawa Ally ( 55) akiwa wodini katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro leo baada ya kujeruhiwa kwenye ajali ya basi dogo la wasanii wa Kundi la Five Stars Moden Taarab la Jijini Dar es Salaam. Yeye alikuwa msanii mwalikwa kwenye safari hiyo ya kikazi katika mikoa ya nyanda za juu kusini .



Na Mwandishi Wetu,Morogoro


NI VIFO vya masikitiko vya wasanii 13 wakiwemo wanaume kumi na wanawake watatu wa kundi la Muziki la Five Star’s Modern Taarabu ambao wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa kati yake mmoja vibaya baada ya gari yao aina ya Toyota Coaster waliyokuwa wakisafiria kutoka Mbeya, kuelekea jijini Dar es salaam kuacha njia na kulivaa lori lililokuwa limesimama na kupinduka, wakikwepa kukutana uso kwa uso na lori lingine lililokuwa likija mbele.

Katika ajali hiyo iliyothibitishwa na Mkuu wa Usalama Barabarani (RTO)Mkoa wa Morogoro Ibrahim Mwamakula, zilibainisha ajali hiyo kutokea Machi 21, majira ya saa 2.30 usiku, ndani ya eneo la hifadhi ya taifa ya Mikumi, kilometa takribani sita kutoka lango kuu la kuingilia hifadhi hiyo ya mikumi kutoka upande wa Doma.

Kwa mujibu wa Mwamakula aliyefika eneo la tukio na hospitali kusaidia kuhifadhi miili ya watu hao, chanzo cha ajali hiyo ni Mwendo kasi wa gari hiyo aina ya Costa iliyokuwa imewabeba wasanii ,yenye namba za usajili T 351 BGE iliyokuwa ikiendeshwa na Juma Hassan anayedaiwa kutoroka baada ya ajali, na uzembe wa dereva huyo kujaribu kulipita gari jingine bila kuwa na uangalifu.

Ajali hiyo ilitokea baada ya Costa hiyo kujaribu kulipita lori aina ya scania lililokuwa limebeba mbao lililokuwa limesimama barabarani baada ya kuharibika lenye namba za usajili T 848 APE na tela namba T 556 BDL mali ya Meshack Rajab Mvamba, na kukutana mbele yake na lori aina ya scania lenye namba T 182 BKB na tela namba T 530 BHY ambalo katika kuikwepa Costa hiyo na lenyewe lilipinduka.

Costa hiyo ilichuna upande mmoja wa lori la mbao, na lenyewe kuharibika upande huo vibaya na kupinduka.

Akizunmgumza kwa masikitiko huku machozi yakimtoka na waandishi wa habari Raisi wa bendi hiyo Ally Juma (25) maarufu kama “Ally J” ambaye ni miongoni mwa majeruhi walionusurika,alisema gari hiyo ilikuwa na watu 24 wakiwemo wasanii 21, madereva wawili na abiria mmoja, na walikuwa wakitokea Mkoani Mbeya kwenye maonesho ambapo Jumapili walifanya wilayani Kyela mkoani humo na kabla, siku ya Ijumaa walifanya maonesho Makambako, Mikumi siku ya alhamisi na Kilosa Mkoani Morogoro siku ya jumatano.

Miongoni mwa waliopoteza maisha yumo mwanamuziki Issa Kijoti na kiongozi wa bendi hiyo Nassoro Madenge ambaye ndugu, jamaa na marafiki zake walijitokeza kwa wingi usiku huo katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya mkoa wa Morogoro wakitokea jijini Dar es salaam,na kukesha hadi majira ya saa 10 alfajiri wakiendelea kusaidia zoezi la kushusha miili iliyokuwa imeharibika vibaya kwa kuchanwa na kukatika baadhi ya viungo.

Wengine waliokufa katika ajali hiyo ni waimbaji wa bendi hiyo Husna Mapande na Hamisa Omary ambaye ni mke wa msanii Mussa Mipango, mpiga solo Shebe Juma, mpiga gitaa la base Omary Hashim, mbeba vyombo Omary maarufu kama Tolu,Mfanyakazi wa bendi hiyo Ngereza Hassan, wapiga kinanda Tizzo Mgunda na Hamma Kinyoya, mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Maimuna na mcheza shoo wa kundi la “Kitu Tigo” la Ilala ambaye jina lake halijaweza kujulikana mara moja na hao wote walikufa papo hapo katika eneo la ajali.

Mwingine aliyekufa akipelekwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu ni Haji Mzaniwa (32) mkazi wa jijini Dar es salaam ambaye ni mbeba vyombo katika bendi hiyo.
Majeruhi katika ajali hiyo waliolazwa katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro ni pamoja na mwimbaji Mkongwe na mgeni aliyekuwa amefanya onesho moja tu katika bendi hiyo, Bi Mwanahawa Ally (55), Suzana Benedict (32),Zena Mohamed (27), Samila Rajab (22), Ally Juma (25), Rajab Kondo (25), Mwanahawa Hamis (38), Shaban Hamis (41) na Msafiri Mussa (22) wote wasanii na wakazi wa jijini Dar es salaam.

Mwandishi wa habari hizi alifika eneo la tukio majira hayo ya usiku, na kukuta msururu mrefu wa magari zaidi ya 100 yakiwa yamekwama katika pande zote za njia na kushindwa kupita upande mmoja kwenda mwingine kutokana na ajali hiyo kuzuia njia, huku jitihada za kuwaokoa maiti waliokuwa wamenasa katika Costa hiyo zikiendelea kufanywa na askari wa hifadhi ya Taifa ya Mikumi, watu waliokuwa ndani ya magari yaliyoshindwa kupita na askari polisi waliofika muda mchache baadaye wakiongozwa na Mwamakula.

Aidha baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo,Mohamed Hawanga ambaye ni mfanayakazi TANAPA katika Hifadhi ya Mikumi, Justine Simon aliyekuwa safarini kuelekea Mafinga na Jatemi Lembilinyi aliyekuwa akielekea Iringa wakitokea Dar es salaam, walisema kama sio jitihada za dereva wa lori lililokuwa likija mbele ya costa kukwepesha gari hiyo na kuipeleka porini, huenda angekutana na Costa hiyo uso kwa uso, na watu wote wangeweza kupoteza maisha katika tukio hilo.

Mwandishi wa habari hii alishuhudia msururu wa magari zaidi ya 100 ambayo yalikuwa mengine yakielekea katika mikoa ya Iringa,Mbeya na nchi za jirani,wakati nyingine zilikuwa zikiteleka Morogoro,Dodoma,Dar es salaam yaliyokuwa katika eneo lililotokea ajali hiyo.

Kutokana na ajali hiyo baadhi ya mashibiki na wadau wa muziki wa taarabu mkoani Morogoro wamesikitika kutokea kwa ajali hiyo na hasa kifo cha msanii chipkizi Issa Kijoti aliyetamba na wimbo wa ‘Msitujadili’ wenye vonjo vya Mchumu Mchumu mwaaa.

2 comments:

  1. wengi tunaamini sana amri ya mungu lakini kusema kweli ajali nyingi za inchini huwa zinaweza kuzuilika, ajali hii inatisha sana, inaweza kuwa dereva alisinzia au alikuwa na haraka za hovyo. kwa wafiwa wote m-mungu awaongezee imani na uvumilivu!!!!

    ReplyDelete
  2. this is sadness time i never see in ma life! but nawaombea allah awape wepesi ktk hii safari yao ya mwisho na pole nyingi kwa wafiwa wote.

    ReplyDelete

Post Bottom Ad