Thursday, July 24, 2014

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AFUNGUA MKUTANO WA 45 WA CPA JIJINI ARUSHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wajumbe wa Chama cha Wabunge kutoka nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC jijini Arusha. Mheshimiwa Makamu wa Rais alifungua mkutano wa 45 wa CPA unaozikutanisha nchi za Afrika unaofanyika nchini Tanzania kuanzia leo Julai 24 hadi Julai 27, 2014. Mkutano huo sambamba na masuala mengine pia unajadili juu ya wajibu wa mabunge na mchango wao katika kusimamia utawala bora pamoja na kusaidia serikali za Afrika kubuni mipango ya maendeleo inayolenga vizazi vya sasa kwa lengo la kuijenga Afrika ijayo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Makamu wa Rais wa CPA na Spika wa Ufalme wa Lethoto, Enoch Sephir Motanyane, wakati akiondoka nje ya ukumbi wa AICC baada ya kufungua rasmi mkutano wa 45 wa CPA unaozikutanisha nchi za Afrika unaofanyika nchini Tanzania, jijini Arusha kuanzia leo Julai 24 hadi Julai 27, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na baadhi ya Wabunge wakati akiondoka nje ya ukumbi wa AICC jijini Arusha baada ya kufungua rasmi mkutano wa 45 wa CPA unaozikutanisha nchi za Afrika unaofanyika nchini Tanzania, kuanzia leo Julai 24 hadi Julai 27, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Spika wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda na Mwenyekiti wa CPA Tawi la Tanzania, Azan Zungu, wakifurahia ngoma ya asili wakati walipokuwa wakiwasili kwenye ukumbi wa AICC, jijini Arusha kufungua mkutano wa 45 wa CPA unaozikutanisha nchi za Afrika unaofanyika nchini Tanzania, kuanzia leo Julai 24 hadi Julai 27, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wabunge baada ya kufungua rasmi mkutano wa 45 wa CPA unaozikutanisha nchi za Afrika unaofanyika nchini Tanzania, kuanzia leo Julai 24 hadi Julai 27, 2014. Picha na OMR


WATOTO WAISHIO KATIKA MAZINGIRA MAGUMU WA KITUO CHA CHILD IN THE SUN WAPEWA MSAADA WA VIFAA VYA SHULE NA TCAA

Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)Ally CHangwila akimkabidhi msaada wa Madaftari na vyakula mbalimbali Samson Ali (12) ambaye ni mmoja wa watoto waishio katika mazingira magumu ambao hivi sasa wanalelewa katika Kituo cha Child In The Sun kilichopo Manzese Dar es Salaam kituo hicho kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki.watoto hao wanapatikana kwa kukusanywa mitaani.
Mwalimu wa Kituo cha Kulea watoto waishio katika mazingira Magumu cha Child In The Sun kilichopo Manzese Dar es Salaam, Martin Modest akipokea Msaada wa Vyakula na Vifaa vya Shule yakiwemo Madaftari kutoka kwa Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Ally Changwila ,Watoto hao wanapatika kwa kukusanywa kutoka mitaani na kulelewa hapo ambapo wanapatiwa ushauri kabla ya kuanzishwa shule.
Watoto wanaolelewa katika kituo cha kuleya watoto waishio katika mazingira magumu cha Child In The Sun kilichopo Manzese Dar es Salaam, wakifurahia madaftari waliyokabidhiwa msaada na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania. Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)Ally CHangwila ambaye ndiye aliyekabidhi msaada huo.
Watoto wanaoishi katika Mazingira magumu ambao wanalelewa katika kituo cha Child In The Sun kilichopo Manzese Dar es Salaam, kikiwa chini ya Kanisa Katoliki wakibeba mizigo ya vyakula mbalimbali na vifaa vya shule baada ya kukabidhiwa msaada na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Idd.


Kampeni ya ugawaji wa vyandarua vya hati Punguzo April 2015

Na Lorietha Laurence-Maelezo

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeandaa kampeni kwa ajili ya ugawaji wa vyandarua vya hati punguzo katika kaya nchini, inayotarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka 2015.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Dkt Kebwe Stephen, amesema kampeni hiyo imeanzishwa ili kuziba pengo kutokana na kusitishwa kwa huduma ya hati punguzo iliyokuwa ikifadhiliwa na Mennonite Economic Development Associates (MEDA) mapema mwezi Juni 2014 .

Dkt. Kebwe aliongeza kuwa jamii pamoja na wakina akinamama wajawazito watanufaika na kampeni hiyo, ikiwemo ile ya ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi shuleni ambayo imeanza kutekelezwa tangu mwaka 2013 kwa mikoa ya Lindi,Ruvuma na Mtwara.

“kampeni hii ni muhimu na ni mojawapo ya njia mbadala ya kuendelea kuwasaidia akinamama wajawazito na watoto wachanga kujikinga na ugonjwa wa malaria ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo vya akinamama na watoto”alisema Mhe.Dkt. Kebwe Aidha, jumla ya vyandarua milioni 13 vimesambazwa kupitia mpango huo, ambapo imechangia katika kuongeza matumizi ya vyandarua kwa akinamama wajawazito kutoka 16% mwaka 2004 hadi 75% mwaka 2012 na kutoka 16% hadi 76% kwa upande wa watoto.

Pia alifafanua kuwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua itaendelea kutolewa Kwa watumiaji wa vyandarua hivyo, kwani baadhi ya watu wamekuwa wakitumia tofauti kwa kufugia kuku na hata wengine kuweka katika bustani ili kukinga ndege waharibifu badala ya kujikinga na mbu.

Mpango huu wa hati punguzo ni mkakati ulioendelevu kuhakikisha kuwa makundi ya akinamama wajawazito na watoto wachanga wanaendela kupata vyandarua ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria na umekuwa ukitekelezwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria, Shirika la Maendeleo la Serikali ya Watu wa Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) na Idara ya Maendelao ya nchi ya Uingereza.


Taasisi ya Handeni Kwetu Foundation kuzinduliwa August 5

SIKU chache baada ya kusajiliwa rasmi chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Taasisi inayojulikana kama Handeni Kwetu Foundation, imepangwa kuzinduliwa August 5 mwaka huu, katika Ukumbi wa Vijana Social Hall, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kutafuta namna ya kusaidiana na serikali katika mambo mbalimbali, ikiwamo Kujenga uwezo kwa jamii kujikwamua kiuchumi na kuhamasisha utawala.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa taasisi hiyo, Kambi Mbwana, alisema taasisi hiyo imeanzishwa na itafanya kazi zake bila kuvunja masharti yaliyowekwa na serikali ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanapatikana.

Alisema kuwa taratibu za kuelekea kwenye uzinduzi huo zinaendelea kuwekwa katika hali ya kukutana pamoja kwa wageni walioalikwa kushuhudia uzinduzi huo wa aina yake.

“Kwa miezi kadhaa sasa taasisi ilikuwa kwenye mchakato wa usajili wake, hivyo baada ya kukamilika, kinachofuata sasa ni kuzindua ili ianze kazi zake kama ilivyokusudia.

“Taasisi hii itakuwa na Makao yake Makuu wilayani Handeni, lakini itafanya kazi zake nchi nzima na huko mbele itakuwa na ofisi katika kila eneo itakaloona inafaa,” alisema.

Sababu nyingine za kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuleta ustawi kwa jamii katika njanya mbalimbali, kutoa mafunzo kuhusu kilimo bora na jinsi ya kutafuta masoko, kutoa elimu ya uraia na kuhamasisha misingi ya utawala bora, kutoa elimu na ushauri kuhusu mbinu bora za kuimarisha  afya na elimu ya msingi kuhusu Virusi vya Ukimwi na Ukimwi.

Malengo mengine ni kutoa elimu kuhusu makundi rika katika elimu ya uzazi, kuhamasisha na kushawishi jamii kuzingatia ustawi wa mtoto katika jamii, kufanya utetezi kwa makundi maalum ambayo haki zao zinakiukwa na kufanya tafiti mbalimbali zenye malengo ya kuboresha maisha ya jamii, kiuchumi na kijamii.


KUWENI MAKINI NA TAASISI ZA FEDHA FEKI - SERIKALI

Na Rose Masaka-MAELEZO-Dar es Salaam.

Serikali imewataka  wananchi       kujihadhari na wizi ambao hufanywa na Taasisi za Fedha hewa ambazo zimekuwa zikidai kutoa mikopo kwa njia ya simu.

Tahadhari hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Assah Mwambene wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa Taasisi hizo zimekuwa zikitumia  mitandao ya simu za mkononi kutapeli wananchi kwa kuwaraghai kuwa watawapatia mikopo.

Mwambene ameongeza kuwa Taasisi hizo zimekuwa zikitumia majina ya viongozi wakubwa mbalimbali wa vyama na Serikali kuwatapeli wananchi kwa kuwachukulia fedha zao.

Amesema kuwa baadhi ya taasisi hizo zinatumia namba za uongo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaibia wananchi.

Mkurugenzi huyo amezitaja baadhi ya Taasisi hizo kuwa ni pamoja na Social credit Loans ambayo inadai  imesajiliwa na TRA kwa namba Reg.No.33/SCC/REG/7894 na namba ya utambulisho wa mlipa kodi ni TIN:203-344-6789.

Taasisi nyingine ni Saving Foundation na Quicken Loan ambazo zote hizo zimekuwa zinawatapeli wananchi.

Amesema kuwa baada ya kuwasiliana Mamlaka ya Mapato Tanzania, imebainika kuwa hakuna taarifa yoyote kuhusu Taasisi hizo. 

Mwambene amesema kuwa Serikali inaendelea kufanyia uchunguzi ili wahusika waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua.

Aidha , Mkurugenzi huyo amewakumbusha wananchi kutokubali maombi ya fedha, fadhila au maelekezo yanayodaiwa kutolewa na uongozi wa juu bila kupata uthibitisho kutoka mamlaka husika.


BENKI YA MAENDELEO YAZINDUA MAENDELEO BANK INSURANCE AGENCY

Mkurugenzi mtendaji wa Maendeleo Benki,Ibrahim Mwangalaba (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa UAP,Nick Itunga kwa pamoja wakifunua pazia kuashiria uzinduzi wa huduma hiyo.
 Wakurugenzi wakifuatilia jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
 Mkurugenzi mtendaji wa Maendeleo Benki,Ibrahim Mwangalaba (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa UAP,Nick Itunga kwa pamoja wakifunua pazia kuashiria uzinduzi wa huduma hiyo.
 Mkurugenzi mtendaji wa Maendeleo Benki, Ibrahim Mwangalaba (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa UAP,Nick Itunga kwa pamoja wakipeana mikono baada ya Uzinduzi.
 Mkurugenzi Mtendaji wa UAP,Nick Itunga akizungumza na waandishi  wakati wa Uzinduzi.
 Viongozi wa Maendeleo Banki wakifuatilia jambo wakati wa Uzinduzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Benki, Ibrahim Mwangalaba akizungumza wakati wa Uzinduzi.


Rais Kikwete afungua ujenzi wa barabara Tunduru - Mangaka matemanga,pia azindua mradi wa maji Nalasi -Tunduru

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) na balozi mdogo wa Japan nchini Kazuyoshi Matsunaga (wa tatu kushoto) wakishirikiana kukata utepe ikiwa ni ishara ya kuzindua ujenzi wa Barabara ya Tunduru-Mangaka Matemanga mradi unaojengwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la kimataifa la maendeleo JICA.Wengine pichani toka kushoto ni ni Mbunge wa Nanyumbu Dunstan Mkapa,Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Kapten Mstaafu Joseph Simbakalia,Waziri wa ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete,Wairi wa Ardhi nyumba na mendeleo ya makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa TAMISEMI,Hawa Ghasia.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza balozi mdogo wa Japan Kazuyoshi Matsunaga muda mfupi baada ya kuzindua ujenzi wa Barabara ya Tunduru-Mangaka Matemanga mradi unaojengwa na Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la kimataifa la maendeleo JICA.Kushoto ni mbunge wa Nanyumbu Dunstan Mkapa, wapili kushoto ni Waziri wa ujenzi Dkt.John Pombe Magufuli, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na kulia ni Wairi wa Ardhi nyumba na mendeleo ya makazi Profesa Anna Tibaijuka
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akifungua maji katika kisima kuashiria kuzindua rasmi mradi wa maji katika kata ya Nalasi wilayani Tunduru.Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Bakari Nalicho,Wapili kulia anayepiga makofi ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu na kulia ni Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kata ya Nalasi Rehema Kassim Yakubu wakati alipokwenda kuzindua mradi wa maji katika kata hiyo iliyopo katika wilaya Tunduru leo.(picha na Freddy Maro)


TABIA NA TAMADUNI HATARISHI ZINAZOCHANGIA MAAMBUKIZI YA VVU KWA VIJANA ZABAINISHWA

DSC_0092
Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.

Na Mwandishi wetu
Idadi kubwa ya Vijana hususan wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 wanaanza kufanya mapenzi katika umri mdogo jambo ambalo linaashiria hatari ya maambukizi ya VVU ikilinganishwa na idadi ya Vijana wa Kiume.

Akitoa mada kuhusu tabia hatarishi zinazochangia maambukizi mapya ua VVU kwa Vijana katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa, Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias, amesema hadi sasa kuna Asilimia 3.9 ya wasichana wenye umri huo wamepata maambukizi ya VVU ikilingaishwa na asilimia 1.7 ya wavulana.

Kufanya mapenzi pia katika umri mdogo kunachangia kwa kiasi kikubwa mimba za utotoni na kuathiri ustawi wa maisha ya wasichana. Wastani wa watoto wa kike 6,000 huachishwa masomo kila mwaka kutokana na mimba za utotoni.
DSC_0269
Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu akichangia mada iliyotolewa na Afisa Mradi wa Elimu ya Afya na VVU/UKIMWI kutoka UNESCO, Bw. Herman Mathias (hayupo pichani) katika warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.

“Wasichana wengi wamekatishwa masomo kwa ajili ya kupata Mimba za utotoni zinazochangiwa na kufanya mapenzi katika umri mdogo tabia ambayo pia inachangia maambukizi ya VVU”, alisema Bw. Mathias.

Amezitaja tabia nyingine hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU kuwa ni kuwa na wapenzi wengi kwa wakati mmoja, kuwa na wapenzi wenye umri mkubwa na ngono wenzi.
Nyingine ni matumizi duni na yasiyoendelevu ya Kondomu, kufanya ngono wakati umelewa, ngono kinyume na maumbile na ngono ya jinsia moja.

Akichangia suala hilo Mratibu na Mkufunzi wa Redio Jamii kutoka UNESCO, Bi. Rose Haji Mwalimu amesema tamaduni zinazoendelezwa katika jamii pia zinachangia kumuweka msichana katika kundi hatarishi la kupata maambukizi ya VVU.
DSC_0066
Afisa Mipango VVU/UKIMWI kutoka UNICEF, Bi. Alice Ijumbe akitoa mada ya Afya ya Uzazi kwa Vijana na mahusiano yake na maambukizi ya VVU wakati wa warsha ya siku tatu ya Mradi wa SHUGA Redio inayofanyika katika Kituo cha Redio cha Nuru FM mjini Iringa.

Amezitaja tamaduni hizo ikiwa ni pamoja na kumbagua Mwanamke katika majukumu mbalimbali Kijinsia kutokana na tabia inayofundishwa na kutolewa kwa mtu kulingana na jinsi yake.

“Jinsia, Utamaduni na VVU ni masuala yenye mahusiano yanayomuweka Mwanamke katika hali ya hatarishi kupata maambukizi ya VVU, na kubadili tabia si jambo rahisi kwa sababu limejikita katika tamaduni zetu zinazoelekeza majukumu mbalimbali ya mwanamke na mwanaume kijinsia na hivyo kuchangia maambuki ya VVU” amesema Bi. Mwalimu.

Amesema ni jukumu la Wanahabari Vijana kuhakikisha kuwa wanahamasisha kubadilisha tabia hatarishi zinazochangia maambukizi ya VVU ambazo zimemzunguka mwanamke.

Baadhi ya mifano halisi ya kijinsia kwa wanaume na wanawake katika Afrika ikiwemo Tanzania ni kumuona mwanamume kama kiongozi katika kaya, jamii na kuwajibika kufanya maamuzi yote wakati mwanamke huonekana ni mlezi na kulinganishwa na mtoto mdogo.
DSC_0037
Mfano mwingine ni mitala. Mahusiano ya kimapenzi hata katika jamii isiyokumbatia mitala kutoka na tamaduni zilizojikita katika jamii inakubalika kwamba mwanaume ana haki ya kuwa na wapenzi wengi wakati wanawake wanatakiwa kuwa waaminifu kwa mtu mmoja ambao ni waume zao.


Tanzania katika sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Jumuiya ya madola Glasgow, Scotland

 Jina la Tanzania linameremeta wakati wanamichezo wetu walipopita katika maandamano ya ufunguzi wa Michezo ya Jumuiya ya Madola kwenye sherehe kabambe za ufunguzi katika Uwanja wa Celtic Park jijini Glasgow, Scotland, uliobeba watazamaji 40,000 huku watu bilioni 1 wakiangalia live sherehe hizo kupitia katika TV zao. Takriban  mashabiki 100,000, na wanamichezo 4,000 kutoka katika nchi 71 zitakazoshindana wapo hapo kwa michezo hiyo ambapo hii ni mara ya 20 kufanyika toka ianzishwe.
 Sehemu ya wanamichezo wa Tanzania kwenye sherehe hizo za ufunguzi. Jumla ya wanariadha 9 na kocha wao waliweka kambi nchini Ethiopia ikiwa ni jitihada za Serikali za kukuza na kuendeleza Sekta ya Michezo nchini kupitia mpango wa Diplomasia ya Michezo, ambapo wanamichezo mbalimbali wameweka kambi ambao wanamichezo wengine waliweka kambi katika nchi za Uturuki, China na New Zealand
 Tanzania Oyeeeee....!!!!
 Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha nchini Suleiman Mjaya Nyambui (T-shirt ya njano) akihamasisha vijana wake
Nahodha na bondia wa Tanzania Seleman Salum Kidunda akipeperusha juu bendera ya Taifa wakati akiongoza wenzake kwenye maandamano hayo ya ufunguzi.


TIB Development Bank kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuendeleza fukwe za Coco Beach jijini Dar

TIB Development Bank ikishirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imefanya upembuzi yakinifu na kutayarisha michoro kwa ajili ya kuendeleza eneo la ufukweni maarufu kama Coco Beach la jijini Dar es Salaam. 

Mradi huo ujulikanao kama Coco Beach Park utaboresha mazingira na kuongeza vivutio kwenye eneo hilo pendwa kwa wakazi wa Dar es Salaam. Mradi huu utatekelezwa kwa ushirikiano na wabia mbalimbali na utakuwa unamilikiwa na Manispaa ya Kinondoni. 

TIB Development Bank inashirikiana na Manispaa nyingine mbalimbali nchini kutekeleza miradi ya maendeleo mfano Manispaa za Kagera, Moshi, Ilala, Temeke n.k
Mwenyekiti wa Bodi ya TIB Development Bank Profesa William Lyakurwa akiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Mhandisi Mussa Natty wakikata utepe kuzindua mradi wa Coco Beach Park. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TIB Development Bank Bwana Peter Noni.
Bwana Jaffar Machano kutoka TIB Development Bank akiielezea michoro ya mradi wa Coco Beach Park kwa Mwenyekiti wa Bodi ya TIB Profesa William Lyakurwa na Mkurugenzi Manispaa ya Kinondoni Mhandisi Mussa Natty
Muonekano wa Coco Beach Park itavyokuwa baada ya kumalizika mradi.


Neno la Leo Kitaani: Kama ulikuwa Hujui,Uliza

huku kwetu watu wanasafiri Bure kwenye usafiri wa jumuiya.


PPF na MSD wasaini makataba wa makubaliano wa mpango wa "wekeza"

 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio, (Kushoto), na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa, (MSD), Cosmas Mwaifwani, wakiweka saini mkataba wa “wekeza” kwenye hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya MSD, Keko jijini Dar es Salaam, Julai 23, 2014. Chini ya Mkataba huo, zaidi wa wafanyakazi 400 wa MSD wamejiunga na PPF. 
 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio, (Kushoto), akibadilishana hati na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa, (MSD), Cosmas Mwaifwani, baada ya kusaini mkataba wa mpango wa “Wekeza” kwenye hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya MSD jijini Dar es Salaam, Julai 23, 2014
 Mkurugenzi wa Operesheni wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Asumpta Malya, (Kushoto), akikabidhi kadi mpya ya uanachama kwa mwanachama mpya ambaye ni mfanyakazi wa MSD, mara baada ya PPF na MSD kusaini makataba wa mpango wa 'Wekeza" kwenye hafla iliyofanyika makao makuu ya MSD, Keko jijini Dar es Salaam, Julai 23, 2014
 Mkurugenzi wa Operesheni wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Asumpta Malya, (Kushoto), akikabidhi kadi mpya ya uanachama kwa mwanachama mpya ambaye ni mfanyakazi wa MSD
 Viongozi wa PPF na wenzao wa MSD, wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutiliana saini mkataba ambapo MSD na PPF zimekubaliana kuanzisha mpango wa "Wekeza" ambapo wafanyakazi wa MSD sasa watakuwa wakichangia kwenye mfuko huo ili kujiwekea akiba na kujipatia mafao mbalimbali
Viongozi wa PPF na wenzao wa MSD, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa MSD waliokabidhiwa kadi za uanachama wa Mfuko huo, mara baada ya kutiliana saini mkataba ambapo MSD na PPF zimekubaliana kuanzisha mpango wa "Wekeza" ambapo wafanyakazi wa MSD sasa watakuwa wakichangia kwenye mfuko huo ili kujiwekea akiba na kujipatia mafao mbalimbali


 
Modified by MKCT
Nafasi Ya Matangazo
Idadi ya watu
Idadi ya watu